Bei ya nyama mnadani kuuzwa kwa vipimo

20Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Bei ya nyama mnadani kuuzwa kwa vipimo

WAZIRI wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amesema kuanzia sasa minada ya nyama inayojengwa itakuwa na mizani ili kuondokana na upangaji wa bei kwa kukadiria kwa macho na kumnyima faida mfugaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto), akifungua mkutano wa wadau wa kuku wanyama, jijini Dar es Salaam juzi. Kulia ni Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama, Imani Sichalwe. PICHA: MIRAJI MSALA

Aliyasema hayo jana alipokutana na wafugaji wa kuku wa nyama, wauzaji wa vifaranga na vyakula ili kusikiliza kero ambazo mojawapo walitaja ni kukosa faida kutokana na mauzo ya kuku kwa sababu ya kuuzwa kwa kukadiriwa kwa macho.

Katika kero hiyo, wafugaji hao waliomba serikali iruhusu wauze kuku kwa kilo kuanzia shambani.

Waziri Ndaki alisema upangaji wa bei kwa macho bado uko katika minada mingi ya mazao ya nyama na kueleza kuwa ili kuondokana na tatizo hilo, wameamua kila mnada unaojengwa lazima uwe na mzani.

“Tunatakiwa tutoke huko si kwa kuku peke yake hata mazao mengine. Hii ndiyo itatoa faida kwa mfugaji. Minada tutakayojenga itakuwa na mizani ili tuuze kwa kilo. Kuhusu ombi lenu kuanzia, sasa ruksa wafugaji wa kuku wa Dar es Salaam na Pwani kuuza kuku kwa kilo, bei iamliwe na soko,” alisema.

Kuhusu ombi la wafugaji la serikali kuwaondoa madalali wa kuku eneo la TAZARA jijini Dar es Salaam ambao wamekuwa wakiuza vifaranga kwa bei juu na wengine wasio na viwango, Waziri aliwaagiza watendaji walishughulikie ikiwezekana wafikishwe kwenye vyombo vya dola.

Pia waziri aliwataka watendaji wake waache kujifungia ofisini badala yake waende mtaani kufuatilia wale wanaofanya biashara ya utotoleshaji vifaranga bila kusajiliwa kwa sababu wamekuwa wakisababisha hasara kwa wafugaji kwa kuwauzia visivyo na ubora.

Kwa upande wa ubora wa chakula cha kuku, aliwataka wataalamu badala ya kusubiri kuletewa kwenye maabara ili wapime ubora, waende mtaani kukagua.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kuku wa Nyama (TABROFA), Costa Mrema, aliainisha mambo sita wanayoomba serikali iyafanyie kazi. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuwapo kwa machinjio ya kuku, kupandishwa bei ya vifaranga muda mfupi kwa kampuni zinazototolesha na kulazimishwa kununua chakula na kampuni za uuzaji kuku.

Naye Mkuu wa Maendeleo ya Biashara kutoka kampuni ya AKM Glitters, John Baitani, alitaja matatizo mengine kuwa ni kodi na tozo mbalimbali zinazofikia 42 wakati wa uingizaji nchini mitambo inayohusiana na ufugaji kuku.

Habari Kubwa