Bei ya pamba yakwamisha kampuni kununua

15Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Kahama
Nipashe
Bei ya pamba yakwamisha kampuni kununua

KUSUASUA kwa soko la zao la pamba wilayani Kahama mkoani Shinyanga, kumedaiwa kutokana na kushuka kwa bei ya soko la dunia na kusababisha kampuni ya ununuzi kushindwa kununua kwa kuogopa kupata hasara.

Akizungumza jana na vyombo vya habari, Meneja wa shughuli wa zao la pamba kutoka Chama Kikuu cha Ushirika (KACU), Amri Mwinyimkuu, alisema mpaka sasa kati ya kampuni nne zilizopatiwa leseni ya ununuzi wa zao hilo ni mbili zilizoanza kununua pamba.

Alisema, bei iliyopitishwa kwa ajili ya kununua zao hilo ilikuwa ni Sh. 1,200, lakini kabla hawajaanza kununua ikaporomoka na kufikia Dola la Kimarekani 63 kwa pamba nyuzi, sawa na Sh. 1,449.

Pia alisema, kwa mkulima bei ya pamba bado haijashuka isipokuwa kampuni zinalalamika bei ya pamba nyuzi inazidi kushuka katika soko la dunia, nakuongeza endapo watanunua kwa bei Sh. 1,200 serikali iwapatie fidia ya hasara watakayoipata.

Hata hivyo, alisema bei ya pamba nyuzi katika soko la dunia imeporomoka kutoka Dola 1.53 hadi kufikia 1.39 kwa kilo moja, na kuongeza hali hiyo ndiyo inayosababisha kampuni nyingi kushindwa kupeleka fedha kwenye vyama vya msingi kununua.

Vile vile, Mwinyimkuu alisema, kati ya asilimia 33 hadi 35 huwa ni pamba nyuzi kwenye pamba mbegu, huku asilimia 62 hadi 65 huwa ni mbegu na kuongeza asilimia mbili inayobaki huwa ni uchafu ambao huwa unatupwa.

Kadhalika alisema kwa mwaka huu wanatarajia kupata zaidi ya kilo milioni 4.7 ikilinganishwa na mwaka jana walipata kilo milioni 2.3 na kuongeza zaidi ya wakulima 13,559 kutoka katika Halmashauri ya Ushetu, Kahama mjini na Msalala wamelima zao hilo.

Mkagunzi wa pamba wilayani hapa, Emmanuel Kileo, alisema, kati ya kampuni nne zilizopewa leseni ya ununuzi wa zao hilo, ni mbili tu zimejitokeza kununua zao hilo ambazo ni Fresho na Kaham Oil Mill.

Vile vile, Kileo alisema kwa sasa wakulima wanapeleka matolori ya pamba sehemu ambazo wamesikia kampuni hizo zimepeleka fedha na wakati mwingine wanakuta fedha zimekwisha na hali hiyo itasababisha wakulima kushindwa kulipa madeni ya pembejeo.