Bei ya samaki yapaa

15Feb 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Bei ya samaki yapaa

SAMAKI na dagaa katika Soko Kuu la Samaki la kimataifa Feri jijini Dar es Saam wamekuwa adimu na kusababisha bei zake kupanda mara dufu.

Umati wa wachuuzi wa samaki wakiwa kwenye mnada katika Soko la Samaki la Kimataifa Feri, jijini Dar es Salaam jana, ambapo kitoweo hicho kilionekana kuwa adimu na kusababisha bei yake kupaa. PICHA: ROMANA MALLYA

Bei ya ndoo kubwa ya dagaa wa aina mbalimbali wanaovuliwa Bahari ya Hindi kwa sasa ni kati ya Sh. 80,000 hadi 85,000 huku samaki walio wengi waliopo sokoni hapo wanatokea visiwa vya Mafia na Kilwa.

Nipashe ilifika jana kwenye soko hilo na kushuhudia hali ya upatikanaji wa samaki na dagaa imepungua, huku maofisa uvuvi na wavuvi wenyewe wakitaja sababu ni kipindi cha mbalamwezi.

Akizungumza na gazeti hili sokoni hapo, mmoja wa wauzaji wa dagaa, Adam Issa, ambaye ni mkazi wa Manzese alisema, bei ya dagaa sokoni hapo hadi siku hiyo kwa ndoo kubwa ni Sh. 85,000 wakati kwa kawaida huwa ni Sh. 25,000.

“Kwa kawaida ndoo kubwa ya dagaa huwa kati ya Sh. 25,000 hadi 30,000 lakini kwa sasa ndani ya wiki moja iliyopita imepanda na inauzwa kati ya Sh. 80,000 hadi 85,000. Ukinunua kwa fungu kwa sasa ni kati ya Sh. 2,000 hadi 5,000 wakati awali lilikuwa ni Sh. 1,000 hadi 2,000. Hii inatokana na upatikaji wake kuwa shida.

Issa alisema uhaba huo wa dagaa licha ya kuwaathiri walaji kwa kushindwa kumudu bei, wamekuwa wakikaa nazo sokoni na wakati mwingine kupata hasara.

“Awali, ukinunua ndoo kama hii saa 1:00 asubuhi saa mbili mbele imekwisha lakini kwa sasa unaweza kupita siku hujamaliza kuuza, hii ni hasara kwa sababu tunauza wakiwa wabichi,” alisema.

Akielezea hali hiyo, Ofisa Uvuvi sokoni hapo, Mwajuma Moyo, alisema changamoto hiyo imedumu kwa muda wa wiki sasa kutokana na kuwa kipindi cha mbalamwezi au mwezi mkali.

“Kipindi cha mbalamwezi ni kwamba kuanzia giza linapoanza kuingia kunakuwa na mbalamwezi mpaka asubuhi, ikitokea hivyo wavuvi wenye vifaa vya uvuaji kuviegesha feri kwa sababu ni vigumu kupata samaki au dagaa kwa wingi unaotakiwa.

Alisema vyombo vinavyokwenda kuvua ni vichache na hutumia aina nyingine ya mitego kama mishipi.

“Hali hii imeathiri pia wafanyabiashara hususani wanawake ambao kwa wingi hufika sokoni hapa kila siku kununua dagaa na samaki ili kwenda kuwauza mtaani, kutokana na changamoto hii bei imekuwa juu zaidi na kufanya washindwe kuimudu,” alisema.

Alisema inapokuwa hali ya hewa ya kawaida, uvunaji wa dagaa kwa siku sokoni hapo huwa ni tani 48 hadi tani 50, lakini kwa sasa ni kidogo sana.

Kwa upande wa samaki, alisema wengi kwa sasa wanatoka Kilwa na Mafia ambao huletwa wakiwa wamehifadhiwa kwenye mabarafu.

“Ingawa na wao ni wachache kwa sababu hata huko hali ya upepo ni kama huku, upatikanaji ni tatizo bado hadi sasa bado hatuna samaki wa kutosha na bei zake nazo zipo juu,” alisema.

Moyo alisema kwa mfano kwa sasa samaki aina ya changu anauzwa kati ya Sh. 12,000 hadi 13,000 wakati awali bei ilikuwa ni Sh. 8,500 hadi 9,000.

Pia alisema kwa upande wa samaki aina ya tasi kwa sasa anauzwa kati ya Sh. 8,000 hadi 9,000 wakati awali alikuwa ni Sh. 6,000.

Habari Kubwa