Bei za vifaa vya shule zawatoa jasho wazazi

08Jan 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Bei za vifaa vya shule zawatoa jasho wazazi

WAKATI maandalizi ya kuanza kwa mwaka mpya wa masomo katika shule za msingi na sekondari yakipamba moto, baadhi ya wazazi wamesema bei ya vifaa imepanda hivyo kuishauri serikali kupunguza ushuru wa vifaa vinavyoingia nchini ili kumudu gharama.

Wakizungumza na Nipashe jana wakati wakinunua vifaa vya shule katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, walisema gharama za vifaa ni kubwa kulinganisha na hali ya kipato cha maisha ya mwananchi wa kawaida.

Tamim Ally, mkazi wa jiji ambaye alikuwa akinunua vifaa vya shule, alisema gharama za mabegi zimepanda hadi Sh. 80,000 katika maduka mbalimbali.

Alisema gharama hizo zinafanana na za mwaka jana isipokuwa wafanyabiashara walikuwa wakipunguza bei.

“Huenda mwaka jana walikuwa wakikwepa kulipa kodi na sasa wanalipa kodi halali na ndiyo sababu yale mambo tuliyozoea ya bei kushuka sana hayapo,”alisema.

Ally alisema vifaa vingi vya shule kama rula, kalamu, mkebe, mabegi na vitabu mbalimbali vinatoka nje ya nchi na kwamba kama serikali itapunguza kodi ni wazi gharama nazo zitashuka.

“Kama serikali imeamua kutoa elimu bure, ina wajibu pia wa kuhakikisha inapunguza gharama za vifaa vya shule ili wazazi wamudu kulingana na matakwa ya kutoa elimu bure. Mfano hapa nimemaliza Sh. 150,000 kwa ajili ya kununua tu vifaa vidogo vidogo kwa watoto wawili. Sasa kama serikali haitaliangalia hili bado kama nchi tutashindwa kupiga hatua,” alisema.

Meneja wa Masoko wa Duka la Vifaa vya Shule la Seifi, Allan Saria, alisema sababu ya kutoa bidhaa hizo nje ya nchi ni kutokana na bidhaa zinazozalishwa nchini kuwa za gharama kubwa.

Naye muuza mabegi eneo la Karume jijini Dar es Salaam, John Mushi, alisema begi moja la dukani linauzwa kwa Sh. 40,000 hadi Sh. 35,000 na yale ya mitumba yanauzwa hadi Sh. 50,000 na kwamba yako ya bei nafuu yanayouzwa hadi Sh. 25,000 kulingana na ubora.

Kuhusu viatu, alisema bei ya kawaida ni Sh. 35,000 na kwamba msimu huu wa kufungua shule wazazi wanajitokeza kwa wingi kununua bidhaa hizo hasa za mtumba.

Habari Kubwa