Benki ya NMB, Zanzibar wakubaliana utunzaji bustani ya Forodhani

23Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Benki ya NMB, Zanzibar wakubaliana utunzaji bustani ya Forodhani

Benki ya NMB imefikia makubaliano na serikali ya Zanzibar kutunza bustani ya Forodhani visiwani humo ikiwa ni moja ya juhudi zake za kuunga mkono azma ya uhifadhi wa mazingira visiwani humo na ajenda ya uchumi wa bluu.

Mkuu wa Biashara ya kadi NMB, Philbert Casmir akiongea kwenye mkutano huo kwenye hoteli ya Serena Inn mjini Zanzibar leo.

Mradi huo wa utunzaji wa bustani ya Forodhani unalenga kuboresha mazingira ya kitalii na kuakisi vyema sifa maarufu ya eneo hilo, na utawezesha bustani hiyo kuvutia wageni wengi zaidi kila mwaka huku ukichangia kuchochea sekta ya utalii.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar leo wakati wa kutangaza Mashindano ya Mbio za Boti Zanzibar yanayodhaminiwa na Benki ya NMB ambayo yanatarajia kufanyika Jumamosi Juni 25,2022, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Simai Msaraka amesema benki hiyo imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo wa serikali ya Zanzibar na imekuwa mstari wa mbele kusaidia mipango mbalimbali ya maendeleo visiwani humo.

Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Hussein Mwinyi imekuwa ikiweka kipaumbele cha kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi na kuzitaka kampuni nyingi kuunga mkono mipango ya maendeleo ya serikali.

"Tumefanya kazi kwa karibu sana na Benki ya NMB katika miaka ya nyuma na nimedhihirisha na kutangaza kuwa tayari tumefikia makubaliano nao ya kuendeleza na kutunza bustani za Forodhani hapa Zanzibar," amesema Msaraka 

Amebainisha kuwa pamoja na kuboresha mandhari ya eneo hilo, mradi huo utaleta manufaa makubwa na kusema, wakandarasi wazawa watazingatiwa huku akionyesha matumaini kuwa mradi huo utasaidia kuboresha sura ya Zanzibar.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Kadi wa NMB, Philbert Casmir wakati wa hafla hiyo amesisitiza dhamira ya benki hiyo katika kusaidia ushirikishwaji wa fedha na kuongeza kuwa benki hiyo itaendelea kutoa bidhaa zinazokidhi matakwa ya wateja.

Amesema mipango ya benki hiyo ni kuendelea kupeleka huduma karibu na wateja huku akiongeza kuwa benki hiyo ina mpango wa kupeleka huduma kwenye maeneo ya Wete, Nungwi, mkoani, Uwanja wa ndege miongoni mwa maeneo mengine visiwani humo.

Aidha, amesema kama sehemu ya dhamira ya benki yake kusaidia ushirikishwaji wa kifedha, Jumamosi hii itazindua Kampeni ya ‘Teleza Kidigitali’ visiwani humo inayotoa huduma za kibenki bila mafadhaiko na suluhu mbalimbali za kibenki za kielektroniki.

Mkuu wa wilaya ya Mjini Unguja, Rashid Simai Msaraka (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na maofisa wa Benki ya NMB baada ya mazungumzo na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena Inn mjini Zanzibar.

“Baada ya uzinduzi wenye mafanikio wa kampeni yetu ya ‘Teleza Kidigitali’ katika mikoa mingi nchini Tanzania, sasa ni zamu ya Zanzibar. Tumejipanga vizuri na kila kitu kipo tayari kwa uzinduzi wa Zanzibar Jumamosi hii hivyo watu wa Zanzibar wajiandae kupata uzoefu wa kipekee wa huduma za kibenki za kisasa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni ya bima ya Britam Insurance wamedhamini mbio za boti za Zanzibar za mwaka huu.

Kampuni hizo mbili zitatoa zawadi kwa washindi zinazofikia shilingi milioni sita na laki tano na zitatoa kifurushi cha bima ya ajali kwa washiriki wote kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Habari Kubwa