Benki ya CRDB na UBA yaidhamini serikali ujenzi wa Stieglers George

15Apr 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Benki ya CRDB na UBA yaidhamini serikali ujenzi wa Stieglers George

BENKI ya CRDB kwa kushirikiana na benki ya UBA zimetoa Sh. trilioni 1.7 kwa ajili ya kuidhamini serikali katika ujenzi wa mradi wa umeme wa Rufiji wa Stieglers George.

Makabidhiano hayo yalifanywa leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, wawakilishi wa serikali, Mkandarasi pamoja na watendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya UBA, Usman Isiaka, alisema kwa mujibu wa masharti ya mkataba huo, umoja huo unahitajika kutoa dhamana za benki za kigeni na za ndani zikiwa ni Sh. trilioni 1.7 kupitia utekelezaji wa mradi  na dhamana ya malipo ya awali kwa mradi huo.

Alisema kwa kuanzia, Benki ya CRDB na UBA zimeshirikiana  na Benki ya Africa Export-Import Bank (Afrieximbank) na benki nyingine za Misri kutoa dhamana za benki kwa Tanesco ambazo zilikabidhiwa jana.

Alieleza kuwa, baada ya kukamilika, mradi huo utazalisha umeme wa megawati 2,100 kuongezwa kwenye gridi ya taifa ambao ni zaidi ya mara mbili ya uwezo wa Tanesco na kusaidia kupunguza tatizo la kukosekana umeme nchini.

“Umeme utakaotokana na mradi huu, utatumia kilovolti 400 mpya  ambao utaunganishwa katika gridi ya umeme ya taifa.  

Alisema serikali ilikuwa na mikakati ya muda mrefu ya kuanzisha kituo hicho cha umeme tangu miaka ya 1960 ambacho kikishatengemaa na kukomaa, kitakuwa ni kituo kikubwa cha umeme nchini na Afrika Mashariki.

Mradi  huo mkubwa unatarajia kuiongezea nguvu Serikali kukabiliana na upungufu wa umeme kwa kuwa uchumi wa nchi na idadi ya watu inaongezeka.

 

Habari Kubwa