Benki ya Dunia yaitaja Tanzania kuingia uchumi wa kati

02Jul 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Benki ya Dunia yaitaja Tanzania kuingia uchumi wa kati

WAZIRI wa fedha na mipango, Dk. Philip Mpango, amesema benki ya Dunia imetangaza kuwa Tanzania ni miongoni mwa tano duniani zilizoingia kwenye kundi la nchi za kipato cha kati kwa kundi la chini mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Mpango amesema kwa mujibu wa benki hiyo, kigezo muhimu cha kwanza cha kutambua nchi zenye uchumi wa kati ni wastani wa pato la mwananchi la kiwango cha kati ya dola za Marekani 1,036(Sh.Milioni 2.3) hadi dola za Marekani 4,045(Sh.Milioni 9.3) kwa kundi la chini.

"Pia dola za Marekani 4,046 hadi dola za Marekani 12,535 kundi la juu, kwa mujibu wa Benki ya Dunia Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zilizoingia kundi la kipato cha kati ambapo nchi nyingine ni Algeria, Sri Lanka, Benin na Nepal," amesema.

Waziri huyo amemshukuru Rais John Magufuli, kwa jitihada kubwa za kukuza uchumi wa nchi na kuiwezesha Tanzania kuingia katika hatua hiyo.

"Hatua hii tuliyofikia ina manufaa mengi, yakiwemo kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa fedha za mikopo ya kibiashara kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kuwa na uhuru na kupanga matumizi na kuondokana na kadhia ya utegemezi," amesema.

Habari Kubwa