Benki ya Exim yamuunga mkono Pinda upandaji wa miti 10,000

16May 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe Jumapili
Benki ya Exim yamuunga mkono Pinda upandaji wa miti 10,000

Benki ya Exim Tanzania imeungana na Waziri Mkuu Mstaafu Mh Mizengo Pinda katika kufanikisha kampeni maalum ya kupanda miti 10,000 katika kata ya Zuzu jijini Dodoma ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhifadhi mazingira.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (picha ya kushoto) akikamilisha zoezi la upandaji wa mti kwa kumwagilia maji. picha ya kulia ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu akimwagilia mti wakati wa zoezi hilo la upandaji miti.

Jitihada za benki hiyo ni muendelezo wa mpango mkakati wake wa kutunza mazingira ujulikanao kama ‘Exim Go Green Initiative’.

Katika kufanikisha kampeni hiyo iliyoratibiwa na taasisi ya Habari Development, benki hiyo pia ilichangia fedha ili kufanikisha ununuzi wa miti katika zoezi hilo lililohudhuriwa na viongozi waandamizi wa serikali ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Waziri Mkuu huyo mstaafu.

Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na  aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge, wafanyakazi wa benki hiyo, walimu, wanafunzi na wananchi wa kata hiyo.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda  akiwaelekeza wafanyakazi wa benki ya Exim kuhusu ufugaji wa samaki wakati wafanyakazi hao walipotembelea miradi mbalimbali ya kilimo, uvuvi na ufugaji kwenye makazi ya Waziri huyo mstaafu jijini Dodoma.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Exim tawi la Dodoma wakiendelea na zoezi hilo la upandaji miti.

Akizungumza wakati watukio hilo, Pinda pamoja na kuipongeza benki ya Exim kwa kufadhili zoezi hilo muhimu, alielezea umuhimu wa kutunza mazingira huku akibainisha baadhi ya changamoto zitokanazo na uharibu wa mazingira kuwa ni pamoja na ukame na mabadiliko ya tabia nchi.

“Ndio maana binafsi nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba  nashirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi kama benki ya Exim ili kwa pamoja tuhakikishe tunaitengeza Tanzania ya kijani’’ alisema Pinda ambae alitumia pia wasaa huo kuwatembeza wageni hao kwenye miradi yake mbalimbali ikiwemo ya kilimo na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano, Stanley Kafu, alisema utunzaji mazingira ni sehemu ya vipaumbele vya benki hiyo na ndio sababu imekuwa mstari wa mbele kubuni na kuunga mkono jitihada mbalimbali za utunzaji mazingira nchini ikiwemo upandaji wa miti na utunzaji wa bustani mbalimbali zilizopo katikati ya miji na majiji mbalimbali hapa nchini.

“Mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa uharibifu wa mazingira yamekuwa na athari kubwa kiuchumi kwakuwa yamekuwa yakizorotesha pia shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na ustawi wajamii kwa ujumla. Ni wazi kwamba hatuwezi kutenganisha athari hizi na ufanisi wa biashara za kibenki,na hiyo ndio sababu tunashiriki kikamilifu katika kutatua changamoto hii,’’ alifafanua.

Alisema kibiashara pia benki hiyo imekuwa ikitoa kipaumbele kwenye utoaji wa mikopo inayohusisha miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira sambamba na kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia ya mawasiliano na utunzaji wa kumbukumbu ili kupunguza matumzi ya karatasi.


Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (kushoto) akijadili jambo na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambae kwa sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge (Kulia), Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Bw Stanley Kafu (Katikati) na wafanyakazi wengine benki hiyo wakati wa zoezi hilo la upandaji miti

Zaidi, aliwasihi wananchi hususani wakazi wa kata ya Zuzu kuzingatia na kuheshimu sheria zinazosimamia na kulinda misitu ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu huku akiahidi kuchimba kisima kwa ajili ya kuwezesha umwagiliaji wa miti hiyo.

Habari Kubwa