Benki ya TADB yazindua baraza la kwanza la wafanyakazi

14Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Benki ya TADB yazindua baraza la kwanza la wafanyakazi

Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imefanya uchaguzi, kuunda Baraza la wafanyakazi na kuzinduliwa kwa Baraza hilo.   

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Frank Nyabundege (wa pili kulia) akimkabidhi mkataba wa kuunda baraza la wafanyakazi Tulia Msemwa, afisa kutoka ofisi ya Kamishna wa kazi muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa baraza la wafanyakazi (workers council) wa benki hiyo jijini Dar es Salaam jana. Wa kwanza kulia ni katibu mkuu aliyechaguliwa Edna Nyatta na wa pili kushoto ni katibu mkuu msaidizi, Abdi Jangawe Msuya

Akitoa elimu kabla ya uundaji wa Baraza, Tulia Msemwa Afisa Elimu Kazi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Kamisha wa Kazi alisema Baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu  mahala pa kazi kwa kuwa ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi na lina mchango mkubwa katika kuleta ufanisi. Alibainisha kuwa Baraza linajukumu la kuhakikisha wafanyakazi wanafahamu haki zao na wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.

“Uundwaji wa baraza la kazi hapa TADB utasaidia kuleta ufanisi kwa taasisi na Taifa kwa ujumla. Ikumbukwe kuwa Serikali inazingatia sana suala la taasisi zake kuwa na mabaraza ya Wafanyakazi kwani yanaanzishwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za idara, taasisi na Wizara kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali watu,” alisema.

Akizungumza wakati wa kusimamia uchaguzi, Muwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi Viwanda, Biashara, Taasisi za fedha Huduma na Ushauri (TUICO) Willy Kibona alipongeza uongozi wa TADB kwa kuamua kuharakisha ukamilishaji wa uundaji wa Baraza la wafanyakazi. Aliendelea kupongeza TADB kwa kushirikisha vyombo vya habari katika mchakato mzima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Frank Nyabundege (aliyesimama) akiongea muda mfupi kabla ya uchaguzi wa baraza la wafanyakazi la benki hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana uliopelekea kuundwa kwa baraza la kwanza la wafanyakazi.

“Hii ni hatua kubwa na niombe taasisi nyingine ziweze kujifunza hapa. Suala la uundwaji wa mabaraza ya wafanyakazi linapaswa kufanyika kwa uwazi. Kipekee niseme kuwa ni mara ya kwanza kuona vyombo vya habari vikishirikishwa katika mchakato kama huu,” alisema Kibona.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege alisema  kuwepo na uwakilishi kamilifu wa baraza la wafanyakazi kutasadia kushauri na kuondoa viashiria vyovyote vya ubaguzi au uonevu katika eneo la kazi na kuongeza ari pamoja na ufanisi zaidi katika utendaji kazi.

“Kuundwa kwa baraza hili muhimu, kutasaidi sana kuwa na njia nzuri na inayokubalika kisheria ya ushirikishwaji wa wafanyakazi na kuwezesha majadiliano yenye tija kwa taasisi yetu na kwa wafanyakazi wake. Pia litasaidia kuweka namna nzuri ya kuboresha mazingira ya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zote katika kujumuisha wafanyakazi katika maamuzi na mipango ya taasisi yetu kuanzia sasa na kuendelea. Nia yetu ni kuona kuwa TADB inakuwa sehemu salama na yenye kufurahiwa kufanya kazi,” alisema

Wafanyakazi wa TADB walipata elimu kabla ya zoezi la uchaguzi wa wakilishi kutoka kila idara na uwakilishi kutoka kanda zote.

Zoezi hili lilikamilishwa na Mkurugenzi Mtendaji ambaye ni mwenyekiti wa Baraza kwa kukata utepe mkataba baina ya Taasisi na Chama cha wafanyakazi kuashiria kuanza kazi rasmi kwa Baraza hilo.

Viongozi wa baraza jipya la wafanyakazi la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wakiwa katika picha ya Pamoja na menejimenti ya benki hiyo Pamoja wawakilishi kutoka TUICO na ofisi ya Kamishna wa kazi muda mfupi baada ya uchaguzi wa baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Frank Nyabundege (wa pili kulia) akikata utepe nakala ya mkataba wa kuanzishwa kwa baraza la wafanyakazi kuashiria uzinduzi rasmi wa baraza la kwanza la wafanyakazi wa benki hiyo. Wa tatu kushoto ni Tulia Msemwa ambaye ni afisa kutoka ofisi ya Kamishna wa kazi na wengine ni wawakilishi TUICO pamoja wafanyakazi wa benki hiyo.

Habari Kubwa