Benki yapunguzia riba wakulima, wafanyabiashara

25Jan 2022
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Benki yapunguzia riba wakulima, wafanyabiashara

BENKI ya CRDB imepunguza riba katika mikopo ya vikundi vya wakulima kutoka asilimia 20 hadi tisa na kwa wafanyabiashara kutoka asilimia 16 hadi 13, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali katika kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), jijini Dar es Salaam jana, kuhusu punguzo kubwa la riba katika mikopo ya kundi la wakulima. Wapili kulia ni Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRBD, Bruce Mwile na Ofisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, punguzo hilo limekuja kufutaia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa benki kupunguza riba ili kuchochea uchumi.

Alisema punguzo hilo linatoa ahueni kwa wateja wa benki hiyo kulipa mikopo yao kwa riba nafuu, viwango vya chini vya marejesho ya awali, pamoja na kupata wigo mpana wa kukopa.

“Kwa ushirikiano mkubwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ambaye ndiye msimamizi wa sekta ya benki nchini, mwishoni mwa mwaka jana tuliweza kukaa chini na kuanza kupitia upya riba za mikopo mbalimbali inayotolewa na benki yetu na hivyo ninajivunia kuona leo hii tumekuja na suluhisho la kilio cha muda mrefu cha wateja wetu,” alisema Nsekela.

Kadhalika, alisema punguzo la asilimia tisa kwa mikopo ya kilimo ilitolewa ili kusaidia kuimarisha sekta ya kilimo ambayo huchangia zaidi ya asilimia 26 ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa asilimia 75 ya Watanzania.

Sababu ya kutoa punguzo hilo alisema kuwa ni kuchochea kasi ya mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima wadogo na wakati kufanya kilimo cha kisasa kupitia mikopo nafuu ya pembejeo na zana za kilimo.

Aidha, alisema kuwa benki hiyo imetoa asilimia 40 ya mikopo yote ya kilimo nchini, huku akibainisha kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, walitoa mikopo ya zaidi ya Sh. trilioni 1.6 kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani katika kilimo, huku akitolea maelezo na kwa upande wa wafanyabiashara pia.

“Wafanyakazi ni kundi muhimu kwa benki yetu ndio maana tumekuwa tukiboresha kwenye riba ya mikopo ya kundi hili kila mwaka ili kuwasaidia kufikia malengo waliyojiwekea jambo ambalo litaongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi, pia msikope bila kuwa na malengo.

“Hii ni mara ya tatu ndani ya miaka mitano iliyopita kwa benki yetu kupunguza riba ya mikopo ya wafanyakazi, matarajio yetu ni kuwa wafanyakazi watachangamkia fursa hii ili kuboresha maisha yao na hilo ndio haswa lengo la Benki ya CRDB,” alisema Nsekela.

Kwa miezi kadhaa sasa serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imekuwa ikitoa wito kwa taasisi za fedha kupunguza riba kwa wateja ili kuimarisha uchumi.

Kufanikisha hilo Benki Kuu imechukua hatua mbalimbali za kisera ikiwamo kupunguza kiwango cha sehemu ya amana za benki kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu, pamoja na kuanzisha mfuko maalum wenye thamani ya shilingi trilioni moja ambao utatumika kukopesha benki na taasisi za fedha kwa riba ya nafuu, ili ziweze kukopesha sekta binafsi.

Habari Kubwa