Betty Mkwasa amchambua Bendera

10Dec 2017
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Betty Mkwasa amchambua Bendera

Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Bahi na Mvomera katika serikali ya awamu ya nne, Betty Mkwasa, amesema alimfahamu marehemu Joel Bendera kama kiongozi aliyependa maendeleo ya jamii.

MAREHEMU Joel Bendera.

Alisema marehemu Bendera, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa mikoa ya Morogoro na Manyara, alikuwa tofauti na wanasiasa wengi ambao huvutia ama upande wao au wa wapiga kura wao kwani alitaka maendeleo kwa ujumla.

"Pia hakuwa mchoyo," alisema Mkwasa, "yeye ndiye alinihamasisha mimi kuanza kulima mpunga." Marehemu Bendera alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati Betty akiwa Mvomero.

"Naomba na viongozi wengine wanaoweza kusaidia wenzao kupiga hatua ya maendeleo (kama marehemu Bendera) wafanye hivyo na wasiwe wachoyo."

Mkwasa alisema hayo jana katika viwanja vya Jeshi Lugalo wakati wa utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Bendera aliyefariki dunia Jumatano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokimbizwa akitokea Korogwe ambako anazikwa huko leo.

Akizungumzia msiba huo, mwenyekiti wa klabu ya michezo ya Bunge na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja alisema wamepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.

Alisema mara ya mwisho kuonana na marehemu ilikuwa katika kikao kilichopita cha Bunge akiwa amefika Dodoma kwa ajili ya shughuli zake binafsi.

Alisema Bendera alifanikisha mafanikio makubwa kwenye soka nchini, hasa katika Bunge ambako aliwezesha Tanzania kuwa bingwa wa Wabunge wa Nchi za Afrika Mashariki.

Aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka (TFF) na mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Leodegar Tenga, alisema marehemu Bendera alikuwa mzalendo na rafiki wa watu wengi hususani sekta ya michezo.

Alisema sekta ya michezo nchini inaweza kumuenzi kwa kutumikia michezo kama ambavyo alikuwa akifanya yeye.Tenga alisema marehemu Bendera alipenda mpira na kuona watu wanaendelea na kufika mbali.

"Alikuwa na kipaji kikubwa cha kuongoza mpira na alitaka kuona watu wakifika mbali katika sekta hiyo," alisema Tenga.

Habari Kubwa