Biashara 16,000 zafungwa miezi 10

16May 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Biashara 16,000 zafungwa miezi 10

SERIKALI imesema uchumi wa Tanzania bado uko imara licha ya biashara 16,252 kufungwa katika miezi 10 iliyopita ya mwaka huu wa fedha.

Imelieleza Bunge kuwa madai kwamba uchumi wa nchi umeyumba kutokana na idadi kubwa ya biashara kufungwa si sahihi.

Akichangia mjadala wa makadirio ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka ujao wa fedha bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji, alijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge na kuelekezwa wizarani kwake, akieleza kuwa takwimu za serikali zinaonyesha biashara zinazofungwa ni chache kuinganisha na zinazofunguliwa.

"Sina sababu ya kudanganya kwa sababu muda wote niko 'field', biashara zilizofungwa na zilizofunguliwa tunazijua. Kuanzia Julai mwaka jana hadi Aprili mwaka huu, biashara zilizofungwa zilikuwa 16,252 na zilizofunguliwa ni 147,818.

"Huo ndio ukweli, kama biashara zimefungwa TRA (Mamlaka ya Mapato) ingewezaje kukusanya kodi? Kama hali ingekuwa hivyo, Tanzania ingekuwa na 'dormant economy' (uchumi uliolala).

"Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi uko imara, uko makini na tunaendelea kutenda kwa ajili ya Watanzania, ndiyo maana tangu Mheshimiwa Rais (John) Magufuli aingie madarakani, hatujawahi kushuka chini ya Sh. trilioni moja kukusanya kodi kila mwezi, huo ndiyo uhalisia tunaoujua," Dk. Kijaji alisema.

Naibu waziri huyo pia alizungumzia suala la kukwama kwa mafuta ya kula bandarini, akieleza kuwa uhalali wa mzigo unapaswa kuthibitishwa na mwagizaji mwenyewe.

"Tunachokifanya ni kufuata taratibu, Watanzania halali wamemwelewa Rais Dk. John Magufuli. Mwaka jana, ombwe kama hili la mafuta lilitokea, lakini lazima tujiulize, kwanini huwa 'wana-target' kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhani?

"Sheria inasema hiki ni chakula, tuonyeshe unatuletea kutoka nchi gani? Kwa 'original documents' (nyaraka halisi) tunataka Watanzania walindwe," alisema.Dk. Ashantu aliongeza kuwa hadi sasa, metriki tani 14,400 za mafuta ya kupikia, nyaraka zake hazijawasilishwa.

"Mafuta hayo yapo, mengine walisema yanatumika nje ya nchi, lakini waliyatoa na kuyaingiza ndani," Dk. Ashatu alisema.

VIWANDA VYA KOROSHO

Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba, alisema msimu ujao, korosho nyingi zitabanguliwa nchini kutokana na wawekezaji wengi kujitokeza kujenga viwanda vya kubangua korosho.

Alisema kangomba ni ujasiriamali ambao sasa unapaswa kutambulika kwa mujibu wa sheria.

"Mambo mengi yanayofanyika, ni kutokana na sheria zilizotungwa hapa bungeni. Kwa mfano, Sheria ya Korosho Namba 12 inasema ukikutwa na korosho kama huna kibali cha Bodi ya Korosho, unapaswa kukamatwa. Tukiamua kufanya kama sheria inavyotaka, hata hao wakulima tutawakamata," alisema.

Mgumba alisema serikali iko kwenye mchakato wa kupitia sheria na Sera ya Kilimo ya Mwaka 2003 ili kuja na sheria na sera yenye kuendana na mazingira yaliyopo.

Alisema kuna wakulima wa korosho wanaoidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 102 kati Sh. bilioni 700, baada ya kuwa imewalipa wakulima zaidi ya Sh. bilioni 600.

Mgumba pia alisema kulinda viwanda vya ndani ni jambo la msingi, lakini si vyote vinafungwa kwa madai ya mipango mibovu ya serikali.

"Kwa mfano, viwanda viwili vya alizeti mkoani Singida vimefungwa kutokana na ukosefu wa malighafi nchini, sasa ni muhimu pia tukahamasisha wakulima katika uzalishaji wa malighafi za kutosha kuviwezesha viwanda," alisema.

Mgumba pia asema serikali iko katika mchakato wa kuingia mkataba maalum na wanunuzi wa mbaazi baada ya kubaini kulifanya makosa ya kutoingia mkataba na wanunuzi wa awali wa zao hilo.

UTITIRI WA MAMLAKA

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, alisema serikali imeanza kuitafutia ufumbuzi changamoto iliyolalamikiwa na wabunge wengi ya utitiri wa taasisi za udhibiti.

"Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Viwanda, imeanza kuchukua hatua. Tayari Waziri Mkuu alikwishachukua hatua kwa kuitisha kikao na kingine amekiitisha Jumamosi ambapo kitapitia changamoto na vikwazo vinavyochangia biashara kutokukua," alisema.Waziri Kairuki alisema zipo tozo ambazo zimependekezwa kuondolewa na kupunguzwa kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha pindi utakapowasilishwa.

Alisema wizara pia imeanza mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji kwa kuwa serikali inatambua sheria hiyo ni ya muda mrefu tangu mwaka 1997 na haiendani na mazingira ya sasa.

Habari Kubwa