Biashara ya saruji kwenda nchi jirani kushika kasi

16Jun 2019
Mary Geofrey
KALAMBO
Nipashe
Biashara ya saruji kwenda nchi jirani kushika kasi
  • Ni baada ya upanuzi wa gati la kisasa kukamilika, katika bandari ya Kasanga wilayani Kalambo mkoani Rukwa

BIASHARA ya saruji kwenda nchi za Demokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi, inatarajiwa kushika kasi na kukuza uchumi wa Taifa, baada ya upanuzi wa gati la kisasa kukamilika, katika bandari ya Kasanga wilayani Kalambo mkoani Rukwa.

Picha za bandari ya Kasanga.

Kwa sasa bandari hiyo ina gati lenye urefu wa mita 20 lenye uwezo wa kupokea meli moja na mpango Mamlaka ya Bandari (TPA) ni kuongeza gati lenye urefu wa mita 100 na kufika mita 120  litakalowezesha kupokea meli tatu za mizigo na abiria.

Meneja wa bandari ya Kigoma anayesimamia bandari zote za Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo juzi, amesema bandari hiyo inategemewa kwa kusafirisha saruji kutoka Mbeya kulekea nchi za Congo na Burundi.

Amesema upanuzi wa bandari hiyo utakaogharimu Sh. bilioni 4.7 utawezesha shehena kubwa ya saruji kusafirishwa kwenda nchi hizo kutoka tani 20,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 kwa mwaka.

"Kuboreshwa kwa bandari hii ya kimkakati inayotegemewa na mikoa ya Katavi, Mbeya, Songwe na Rukwa utawezesha kukuza uchumi wa Taifa. Bidhaa kubwa inayosafishwa kwenda nchi za Congo na Burundi ni saruji ambayo inazalishwa na kiwanda cha Safuri cha Mbeya Cement. Hivyo tunatarajia mizigo itakayosafirishwa inaongezeka mara tano zaidi," amesema  Msese.

Amesema mapato ya bandari hiyo kwa mwaka ni Sh. bilioni moja hivyo wanatarajia yataongezeka mara dufu baada ya kukamilika mradi huo.

Adha, amesema bandari hiyo ambayo ipo Kusini mwa Ziwa Tanganyika, ina ghala la kuhifadhi tani 2,000 za saruji na ghala lingine la nje lenye uwezo kuhifadhi tani 2,000 ya makaa ya mawe.

"Upanuzi wa bandari pia utasaidia shughuli za bandari kufanyika kwa wakati na kuondoa msongamano wa meli zinazosafirisha mizigo kukaa bandarini kwa muda mrefu kwa sababu zote zitafanya kazi kwa wakati mmoja," amesema kiongozi huyo.

Amesema zaidi kuwa, upanuzi wa gati hilo utaenda sambamba na ujenzi wa sakafu ngumu, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi, ghala kubwa la kuhifadhia shehena ya mizigo na ofisi za taasisi za umma zinazofanya kazi na bandari.

Adha, amesema kuelekea katika bandari hiyo kulikuwa na changamoto ya barabara ya kutoka Namanyele kuelekea Kisanga ambayo kwa sasa imeanza kujengwa na Wakala wa Barabara (Tanrods) ili kuongeza ufanisi wa bandari.

Habari Kubwa