Bibi auawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani

28Jun 2022
Neema Sawaka
Kahama
Nipashe
Bibi auawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani

ELIZABETH Kibata (70) , mkazi wa Kitongoji cha Isanagongo, Kijiji cha Nyamigege, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kupoteza maisha papo hapo.

Imedaiwa na ndugu zake kuwa, bibi huyo alivamiwa na watu watatu usiku na mpaka sasa watuhumiwa hao hawajajulikana majina yao na hawajakamatwa.

Mtoto wa marehemu, Lucas Juma (50), akizungumza na Nipashe kwenye kitongoji hicho jana, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa sita usiku.

Alisema kuwa kabla ya uvamizi huo, watu watatu walikwenda kwa marehemu majira ya asubuhi kwa madai ya kutafuta mashamba ya kununua katika familia hiyo.

Juma alisema kuwa baada ya kuvamia walianza kuingia chumba chake na kumwamuru ajifunike shuka na kumtoa mke wake nje na kumnyang’anya simu huku wakimhoji na kisha kumtaka arudi chumbani.

Alisimuliwa kuwa baadaye, watu hao waliingia chumba alichokuwa amelala bibi huyo na wajukuu wawili na kwamba alisikia sauti ya bibi huyo ikimwita lakini aliogopa kuitika.

"Kabla ya kufanyika mauaji hayo, walifika watu watatu majira ya asubuhi, hawakumkuta mama yangu, alikuwa ametoka.
Walimkuta mke wangu ambaye aliwapa majibu hayo na kumwomba namba za simu ili wampigie wajue alipokwenda.

"Baada ya kumkosa waliahidi watarudi tena majira ya saa nane mchana, lakini hawakutokea na usiku ndipo walipovamiwa na kumpiga na kitu kizito kichwani," Juma alisimulia.

Alidai kuwa baada ya kuona kumekuwa kimya, alinyanyuka na kwenda nje kisha kuingia chumba cha mama yake na kukuta sehemu ya kichwa imepondeka ndipo alipopiga kelele na kupiga simu kwa kiongozi wa kitongoji na ndugu wengine kuomba msaada.

Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Sumuni Elias, alisema alipigiwa simu majira ya saa saba usiku na mtoto wa marehemu kuwa wamevamiwa.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema kuwa katika kumdadisi mtoto huyo, alidai kulikuwa na mgogoro wa ardhi katika ukoo upande wa mama yake na watoto wa mjomba wake na kesi ilimalizwa katika baraza la ardhi na kutolewa hukumu.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Anthony Guta, alisema kuwa baada ya kupata taarifa juu ya tukio hilo la mauaji ya kikatili, alitoa amri ya wenyeviti wote wa vitongoji vinne na kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji kuanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wanapoona watu ambao hawawafahamu.

Mwenyekiti wa Waganga wa Tiba za Asili, Kata ya Busangi, Nkwabi Manyesura ( 70), alisema hilo ni tukio la tatu la mauaji ya aina hiyo katika kijiji hicho mwaka huu.

Aliomba serikali kudhibiti matukio ya ukatili kwa kuwa hivi sasa kila akisikiliza vyombo vya habari, anasikia watu wameuawa.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akifafanua kuwa chanzo cha uvamizi na mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi katika familia.

Habari Kubwa