Bil. 100/- zaongezwa malipo ya korosho

08Feb 2019
Godfrey Mushi
Dodoma
Nipashe
Bil. 100/- zaongezwa malipo ya korosho

SERIKALI imesema hadi kufikia jana, ilikuwa imeongeza kiasi cha Sh. bilioni 100 katika fungu la ununuzi wa korosho, hivyo kufikisha jumla ya Sh. bilioni 500 zitakazolipwa kwa wakulima wa zao hilo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi  ya Assumption ya Arusha, Ritta Deo Moshi kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana. Mtoto huyo na wenzake walikwenda bungeni kujifunza shughuli mbalimbali za Bunge. PICHA: OWM

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndiye aliyeyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Mohamed Kuchauka (CCM), wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Kuchauka alikuwa akitaka kauli ya serikali kuhusiana na malalamiko ya wakulima wa korosho ambao hawajafikiwa na uhakiki, licha ya kuwa tarehe ya mwisho inakaribia ukingoni. “Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na songombingo iliyosababisha zao la korosho kwa msimu uliopita, ambao sasa hivi tunaendelea nao wa kukosa soko, jambo lililosababisha serikali kuingilia kati na kutangaza kwamba wangeenda kununua korosho. Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini kauli ya serikali kulingana na hii sarakasi inayoendelea kwenye zao hili la korosho, kwa sababu msimu unakwenda kwisha, lakini bado wakulima malalamiko ni makubwa sana.” Akijibu, Majaliwa, alisema mpaka juzi wa wameongeza Sh. bilioni 100, jambo ambalo linafikisha Sh. bilioni 500 ambazo mpaka sasa serikali imezitoka kwa ajili ya kuwalipa wakulima wa korosho. “Tunachosema si kwamba zao la korosho lilikosa soko, bali lilikosa bei nzuri, soko, wanunuzi wako, lakini walikuwa wakinunua kwa bei ya chini sana kuliko hata ile bei ya kwenye soko la dunia na ilikuwa haimletei faida mkulima. Kwa nia nzuri ya Mheshimiwa Rais (Magufuli), akaamua korosho hizi tununue kwa Shilingi 3,300 bila makato yoyote. “Bodi ya mazao mchanganyiko yenye dhamana kisheria ya kununua mazao na kutafuta masoko popote pale, hasa kwa mazao ambayo yanaonekana kusuasua ilianza kazi yake ya kutafuta fedha na ilifanya tathmini kujua gharama zake. Sasa mpaka jana (juzi) tumeongeza Sh. bilioni 500 kulipa na mahitaji yetu sisi ni Shilingi bilioni 700.” Zaidi, Waziri Mkuu, alisema alilazimika kuingilia kati na kuwapa tarehe ya mwisho ya kulipa wakulima hao, iwe ni tarehe 15 (Februari) na kwamba ana hakika kufikia tarehe hiyo, watakuwa wamelipa madai yote. Aidha, Majaliwa alisema wananchi wote wenye korosho zaidi ya kilo 1,500 watahakikisha kujua kama wana mashamba hata kama muda uliopangwa na kusisitiza kuwa hakuna mkulima aliyekuwapo kwenye orodha ataachwa bila kuhakikiwa. Katika swali jingine aliloulizwa na Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali, kuhusu timu zinazofanya uhakiki wa korosho, hazijawafikia wakulima wenye korosho kuanzia tani moja na nusu, Waziri Mkuu alisema: “Uhakiki wa wakulima hao ulikuwa unafanywa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee na kuwa serikali iliamua kuongeza nguvu kwa kushirikisha mamlaka ya serikali za mitaa. Hizi wilaya zina utofauti wa idadi ya wakulima, kwa hiyo kuanzia Januari 28, mwaka huu walikuwa wameshaanza kujipanga na zoezi hilo halikomi na halitawaacha ambao hawajahakikiwa.”

Habari Kubwa