Bil. 100/- kuleta ajira makinikia

03Aug 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Bil. 100/- kuleta ajira makinikia

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Sunshine ya China imesema inatarajia kutumia Sh. bilioni 100 kujenga hapa nchini mtambo wa kuchenjua mchanga wenye dhahabu, maarufu makinikia, ambao utatoa ajira za moja kwa moja 350.

Makamu Mwenyekiti wa Sunshine hapa nchini, Betty Mkwasa.

Ujenzi wa mtambo huo wa aina yake, pia unatarajiwa kunufaisha maelfu ya Watanzania kwa ajira zisizo za moja kwa moja kwenye fani mbalimbali, wakiwamo pia vibarua, madereva, mamalishe na walinzi.

Makamu Mwenyekiti wa Sunshine hapa nchini, Betty Mkwasa aliliambia Nipashe jana kuwa tayari wameshaanza mazungumzo na serikali na kinachosubiriwa ni kibali cha ujenzi.

Alisema kampuni hiyo ina mtambo kama huo nchini China, hivyo ina uzoefu wa kutosha wa uchenjuaji dhahabu na ndiyo sababu imevutiwa kujenga pia hapa nchini.

“Utaratibu wa kupata kibali kwa masuala kama haya huwa unachukua muda mrefu," alisema Mkwasa ambaye ni Mkuu wa Wilaya mstaafu. "Ila kwa kuwa mazungumzo yanaendelea tuna uhakika serikali itakapotoa kibali tu uwekezaji utaanza mara moja.”

Aidha, Mkwasa alisema kujengwa kwa mtambo huo hapa nchini kutatoa ajira rasmi kwa Watanzania zaidi ya 350 kwa kuanzia; ambao watafanya kazi mbalimbali.

Aidha, Mkwasa alisema kampuni hiyo itajenga mtambo huo eneo lenye dhahabu nyingi ili kupata mchanga mwingi kwa ajili ya kuchenjua, ingawa mpaka sasa hawajachagua eneo rasmi la kuujenga.

“Ingawa mpaka sasa hatujalenga eneo maalum la kuujenga, lakini tutatafuta eneo lenye madini mengi na wakituruhusu tu tutatafuta eneo hilo haraka na mradi utaanza kujengwa,” alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema ujenzi wa mradi huo utakuwa bora na wa uhakika kutokana na kampuni hiyo kuwa na uzoefu wa miaka mingi kwenye uchenjuaji wa madini.

Alisema hata mradi wa uchimbaji wa dhahabu unaofanywa na kampuni hiyo katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, umeonyesha mafanikio makubwa kwani dhahabu inayozalishwa husafishwa na kuwa dhahabu halisi kwa asilimia 99.

“Hao waliokuwa wanatangaza kuwa wakijenga mtambo huo hapa hautalipa hatujui walikuwa wanamaanisha nini," alisema Mkwasa akirejea hoja kuwa ujenzi wa mtambo huo haulipi kibiashara. "Sisi tunaamini kuwa utalipa."

"Sunshine ina uzoefu wa kutosha na ukiangalia dhahabu inayozalishwa Chunya utaona maana inachenjuliwa na kusafishwa hadi inapouzwa inakuwa safi asilimia 99.”

Baadhi ya kampuni za uchimbaji dhahabu ziliwahi kusema kuwa kujenga mtambo kama huo nchini ni gharama kubwa na kwamba hauwezi kurejesha fedha zilizotumika.

Kampuni hizo zilikadiria ujenzi wa mtambo huo ungegharimu dola za Marekani milioni 800 (sawa na Sh. trilioni 1.68).

Rais John Magufuli alipiga marufuku usafirishaji makinikia nje ya nchi Februari, mwaka huu kabla ya kuunda tume mbili kuchunguza kilichomo kwenye makontena 277 ya kampuni ya Acacia, yaliyokamatwa bandarini jijini Dar es Salaam yakiwa njiani kupelekwa nje kwa ajili ya uchenjuaji, Machi 23.

AINA ZAIDI
Aliunda kamati ya kwanza Machi 29,ikiwa na wajumbe nane ambao ni wataalamu wa miamba na kemikali, iliyowasilisha ripoti yake Mei 24 na kubainisha kuwa kwenye makontena hayo kulikuwa na aina zaidi ya 12 za madini mbalimbali ikiwamo dhahabu.
Aprili 10, mwaka huu, Rais Magufuli aliunda kamati ya wataalamu nane wa masuala ya sheria na uchumi kuchunguza thamani iliyomo kwenye mchanga uliopo kwenye makontena hayo 277.

Kamati hiyo iliwasilisha taarifa yake Juni 12 na kubainisha nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya mchanga wa madini inayofanywa na Acacia.

Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.

Hata hivyo, majadiliano kati ya Kamati Maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli na wawakilishi kutoka kampuni ya madini ya Barrick Gold kujadili jambo hilo yalianza Jumatatu Jijini Dar es Salaam, huku Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi akiahidi kusimamia vizuri maslahi ya nchi.

Kampuni tanzu ya Barrick Gold, Acacia ilitoa taarifa mwanzoni mwa wiki iliyopita ikieleza kuwa imepokea kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) hati ya madai ya jumla ya Sh. trilioni 425.

Taarifa hiyo ilisema TRA ilionyesha katika taarifa hiyo kuwa mgodi wa Acacia wa Bulyanhulu unadaiwa kodi ya tangu mwaka 2000 na Pangea unadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.

Habari Kubwa