Bil. 1.5/- kuanzisha utalii wa faru weusi

20Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
SAME
Nipashe
Bil. 1.5/- kuanzisha utalii wa faru weusi

HIFADHI ya Taifa ya Mkomazi itatumia zaidi ya Sh. bilioni 1.5 kuanzisha utalii wa faru weusi utakaokuwa wa kwanza hapa nchini na wa pili duniani, ambao utawawezesha watalii kuwaona kwa karibu wanyamapori hao waliopo hatarini kutoweka.

faru weusi.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Abel Mtui, alisema kuwa aina hiyo mpya ya utalii wa faru inapatikana pekee nchini Afrika Kusini.

 

Mtui alisema Hifadhi ya Mkomazi inakamilisha kazi ya kuzungushia uzio wa umeme katika eneo la kilomita za mraba 13,000 ambalo ndilo litakalotumika kwa utalii huo unaotarajia kuanza rasmi mwezi Julai, mwaka huu.

 

Alisema utalii huo ni tofauti na mradi wa kukuza na kuzalisha faru weusi uliopo ndani ya hifadhi hiyo tangu mwanzoni mwa miaka ya 90 na ambapo ulianzishwa kwa ajili ya kuwaokoa wanyamapori hao waliokuwa hatarini kutoweka.

 

Akifafanua Mtua alisema kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ujangili mwanzoni mwa miaka ya 80, faru weusi walihamishiwa Afrika Kusini na wengine nchi za Ulaya kama Jamhuri ya Czech na baadaye walianza kurudishwa na kuhifadhiwa katika mradi huo wa kuzalisha na kukuza faru.

 

"Kwa kuona uhitaji wa watalii wa kuona faru, Shirika la Hifadhi za Taifa nchini, Tanapa linaanzisha utalii wa faru katika mfumo wa aina yake ndani ya eneo maalumu la kutosha ambalo lina kila kitu kinachohitajika kwa faru," alifafanua.

 

Alisema kazi inayofanyika kwa sasa ni pamoja na kujenga miondombinu ndani ya eneo hilo zikiwamo barabara za kupita watalii, mabwawa ya maji kwa ajili ya wanyamapori hao pamoja na kufunga vifaa vya kisasa vya ulinzi na teknolojia ya kuwafuatilia faru.

 

Mwikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Glory Sumai, alisema faru weusi ni miongoni mwa wanyamapori wanaopatikana nchini ambao wamewekwa katika orodha ya waliopo hatarini kutoweka duniani na Shirika la Kimataifa la Muungano wa Uhifadhi (IUCN).

 

Aliwataja wanyamapori wengine  ni mbwa mwitu na katika hifadhi hiyo pia wameanzishiwa mradi wa kuwazalisha na kuwakuza kwa ajili ya kuwasambaza katika mbuga nyingine za wanyamapori.

 

"Kuanzia mwezi wa saba watalii watakaoingia katika hifadhii hii wataweza kuangalia faru baada ya muda mrefu kuwa na mradi wa kuzalisha faru ambao ulianzishwa kwa lengo la kuhakikisha wanyama hao hawatoweki katika sura ya dunia," alisema.

 

Alisema kutokana na utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (Tawiri), kuanzishwa kwa utalii huo wa faru kutawezesha idadi yao kuongezeka zaidi.

 

Alisema kuwa wanategemea watalii watakuwa wengi kwa kuwa hakuna mbuga nyingine ya wanyamapori ambayo mtu anaweza kuwaona faru kwa uhakika hapa nchini na  nje ya Tanzania.

 

Akizungumzia mbwa mwitu Sumai alisema  idadi yao imeongezeka kwa kuwa hivi karibuni waliingiza katika ikolojia ya Mkomazi na Tsavo Magharibi nchini Kenya zaidi ya mbwa mwitu 200.

Habari Kubwa