Bil. 30/- zatolewa ujenzi kituo biashara kimataifa

26Sep 2021
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Bil. 30/- zatolewa ujenzi kituo biashara kimataifa

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amesema serikali imeanza rasmi ujenzi wa mradi wa Mtaa wa Viwanda na Kituo cha Biashara cha Kimataifa cha Kurasini na tayari Sh. bilioni zimetolewa.

Amebainisha kuwa kampuni tano zimejitoleza kuwekeza kwenye eneo hilo, nne zikitoka nje ya nchi na moja kutoka Tanzania.

Prof. Mkumbo aliyasema hayo juzi mkoani Dar es Salaam wakati wa kutia saini makubaliano na Suma JKT kwa ajili ya ujenzi wa ukuta katika mradi wa ujenzi wa Mtaa wa Viwanda na Kituo cha Biashara cha Kimataifa Kurasini.

Waziri huyo alisema mradi huo utajumuisha mambo matano ambayo ni ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, ujenzi wa viwanda vya kutengeneza na kuunganisha bidhaa mbalimbali na ujenzi wa kituo cha kimataifa cha mauzo ya mazao ya kilimo ikiwamo chai, kahawa, korosho na mboga.

Alisema pia patajengwa maghala ya kuhifadhi katika hali ya uasili na ubaridi bidhaa zinazosubiri kusafirishwa na ujenzi wa kituo cha pamoja cha kutolea huduma (One Stop Services Centre) na huduma za kijamii kama vile ofisi, kituo cha afya na migahawa.

Waziri Mkumbo alisema mwaka huu wa fedha serikali imetenga Sh. bilioni 20 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kujenga ukuta, miundombinu wezeshi ya barabara, maji na umeme.

Alisema watagharamia huduma za mtaalamu mshauri atakayeandaa mpango wa kina wa uendeshaji, kufanya tathmini ya athari za mazingira na usanifu wa kina wa miundombinu.

Alisema mradi huo unatekekezwa kwa mbia kati ya serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA ) na wawekezaji kutoka Sekta Binafsi.

Kiongozi huyo alisema EPZA walishatangaza zabuni ya kukaribisha wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika mradi huo ambao ni: DP World (Dubai); Elsewedy (Misri); Agility (Dubai); Galco (Tanzania); na Shanghai Lingang Group Co. Ltd (China).

Waziri huyo alisema hatua inayofuata ni kwa wawekezaji waliokidhi vigezo vya zabuni kualikwa kuwasilisha andiko la mradi kwa ajili kufanyiwa tathimini na uchambuzi wa kina ili kumpata mwekezaji atakayeshirikiana na serikali katika kutekeleza mradi huo ambao utaanza rasmi Juni mwakani.

Prof. Mkumbo alisema katika mkutano wa ushirikiano kati ya Afrika na China (Sino-Afriva Cooperation) uliofanyika mwaka 2009 jijini Cairo, Misri, pamoja na mambo mengine, Tanzania ilichaguliwa kuwa moja ya nchi nne za Afrika ambazo zingejenga na kuendesha vituo vikubwa vya biashara katika Bara la Afrika.

Alisema katika kutekeleza lengo hilo, serikali ilitenga eneo la Kurasini kwa ajili ya kujenga kituo hicho na uthamini wa eneo na mali ulifanyika mwaka 2013 na malipo ya fidia kukamilika mwaka 2016.

Prof. Mkumbo alisema hadi sasa, serikali imeshalipa jumla ya Sh. bilioni 101 kwa wananchi waliotakiwa kupisha eneo la mradi huo.

"Kufuatia kukamilika kwa malipo ya fidia serikali ilikabidhi rasmi hati ya eneo hilo kwa EPZA Desemba 10, 2019," alisema Prof. Mkumbo na kuitaka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuondoa kitega uchumi chao cha malori katika eneo hilo ili ukuta ujengwe.