Bil. 328/- kutumika sensa ya mwakani

11Jun 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Bil. 328/- kutumika sensa ya mwakani

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema bajeti ya Mwaka wa Fedha 2021/2022, kati ya maeneo muhimu yaliyotengewa fedha ni maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022, ambayo imetengewa Sh. bilioni 328.2.

Dk. Nchemba alisema fedha hizo zitatumika awamu ya kwanza ya sensa, na kwamba sensa hiyo kwa mara ya kwanza nchini, itatumia teknolojia ya vishikwambi (tablets) katika utengaji wa maeneo ya kijiografia na ukusanyaji wa takwimu uwandani.

Alisema matumizi ya teknolojia hiyo mpya yana manufaa makubwa, hasa katika kupunguza gharama na muda wa kukusanya na kuchakata takwimu na kutoa matokeo ya sensa ndani ya muda mfupi.

“Tanzania inajiandaa kufanya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu SURA 351. Kama mojawapo ya maandalizi ya utekelezaji wa Sensa ya Mwaka 2022, Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa upande wa Tanzania Bara.

“Pia Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar imekamilisha kuandaa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka, 2022.

Alisema, kitabu hicho kinaainisha namna ya usimamizi na utekelezaji wa zoezi zima la sensa, gharama ya kufanya sensa pamoja na muundo utakavyokuwa katika ngazi zote za kiutawala.

Dk. Nchemba alitoa wito kwa kamati zote za sensa, wakuu wa mikoa na wilaya zote, wabunge pamoja na wananchi wote, kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha katika maandalizi ya sensa na kujitokeza siku ya kuhesabu watu.

“Lengo ni kuhakikisha watu waliolala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa (usiku wa sensa) wanahesabiwa na kuchukuliwa taarifa zao za kiuchumi, kijamii, mazingira na makazi wanayoishi na mengine mengi, kwa ajili ya kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya wananchi.”

Habari Kubwa