Bil. 400/- kuokolewa kwa uagizaji nje mafuta ya kula

03Aug 2020
Ashton Balaigwa
Simiyu
Nipashe
Bil. 400/- kuokolewa kwa uagizaji nje mafuta ya kula

TAASISI ya Kilimo Tanzania (TARI) imesema imejipanga kuokoa fedha za serikali zaidi ya Sh. bilioni 400 zinazotumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, kwa kuamua kuongeza uzalishaji wa mazao ya michikichi na alizeti.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI. Dk. Geofrey Mkamilo, alisema hayo wakati Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alipotembea banda la taasisi hiyo katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Nyakabindi mkoani Simiyu, ambapo maonyesho hayo yanafanyika kitaifa.

Dk. Mkamilo alisema taasisi hiyo imejipanga kuokoa fedha hizo kwa kuzalisha mbegu bora za michikichi aina ya Tenera pamoja na alizeti ambazo zimeanza kusambazwa kwa wakulima nchini ili kuanza uzalishaji.

Alisema wizara ya kilimo kupitia TARI imedhamiria kutoa mbegu bora za michikichi zitakazotosheleza kupanda hekta 114,000 zilizopo mkoa wa Kigoma zinazofaa kupanda chikichi pamoja na mikoa mingine nchini.

Alisema mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 katika tani hizo tani 205,000 huzalishwa nchini zilizobaki tani 365,000 ndiyo inayoagizwa kutoka nje.

“Kwenye maduka kuna mafuta yanaitwa Korie yamekuwa yakitumika sana kwa wananchi, lakini hilo ni jina la kibiashara lakini mafuta hayo yanatokana na mawese hivyo tunataka kuzalisha michikichi kwa wingi ili tupate mafuta ya mawese,” alisema Dk. Mkamilo.

Alisema wizara pia imepanga mkakati wa zao la alizeti ili kuongeza nguvu ya upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa sababu ni zao la muda mfupi.

“Kuanzia Januari mwakani tunaweka nguvu zaidi kuhakikisha kazi hiyo inakwenda ya uzalishaji wa mbegu bora za mafuta ziweze kuwafikia wakulima,” alisema Dk. Mkamilo.

Alisema kabla ya kuanzishwa kwa TARI Kituo cha Utafiti cha Ilonga kilikuwa kinazalisha wastani wa tani 2.3 za mbegu hizo la alizeti, lakini kwa mwaka wa kwanza baada ya kuundwa kwa taasisi hiyo uzalishaji wa mbegu umeongezeka na kufikia tani 7.5.

Habari Kubwa