Bil.2.4/- zatumika kudhibiti mwendo magari

22Jun 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Bil.2.4/- zatumika kudhibiti mwendo magari

MFUMO wa kuratibu mwenendo au kasi ya mabasi ya abiria nchini hadi sasa umeigharimu serikali Sh. bilioni 2.4, Bunge limeelezwa.

Kazi ya ufungaji wa kifaa hicho kwenye mabasi inafanywa na kampuni ya Bsmart Technologies ya Malaysia, ikishirikiana na kampuni ya Computer Centre ya Tanzania.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, alisema hayo jana bungeni mjini hapa kuwa fedha hizo zimetokana na mapato ya serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Nditiye alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Cecilia Pareso, aliyetaka kujua mfumo wa ‘Vehicle Tracking System’ (VTS) umegharimu fedha kiasi gani, mzabuni wa kazi hiyo kwa nini hakupatikana kwa ushindani kwa kufuata sheria ya ununuzi na je, mfumo huo unaendeshwa kwa kusimamiwa na nani.

Mfumo huo wa VTS ni mfumo unaowezesha upatikanaji wa taarifa mbalimbali za basi likiwa safarini ikiwa ni pamoja na kudhibiti ajali. Taarifa hizo ni pamoja na mwendokasi, mahali basi lilipo, matukio ya ajali na jina la dereva.

Kifaa hicho huchukua matukio na kuyarusha kupitia mfumo wa satelaiti na teknolojia ya ‘Global Positioning System’ (GPS) na kupitia mitandao ya simu yenye teknolojia za ‘Global Packet Radio System’ (GPRS).

"Mzabuni alipatikana kwa njia ya ushindani kwa mujibu wa kifungu cha 150 cha Kanuni ya Sheria ya Ununuzi Tangazo la Serikali namba 446 ya mwaka 2013. Zabuni hiyo ilitangazwa kupitia zabuni ya kimataifa namba EA/025/2015-2016/HQ/G/22 Januari 14, 2016, PPRA Tender Portal, Tanzania Procurement Journal, toleo namba ISS: 1821 VOL IX-No. 3, pia zabuni ilitangazwa kwenye tovuti ya Sumatra," alisema Nditiye.

Kuhusu usimamizi wa mfumo huo, Naibu Waziri Nditiye alisema mfumo huo unasimamiwa na kuendeshwa na Sumatra kupitia kituo maalum kilichoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Ili kuimarisha usimamizi wa mfumo huo, alisema Sumatra imeingia mkataba na kampuni ya Tera Technologies and Engineering kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo kwenye magari.

Habari Kubwa