Bilionea amkana mwanawe kisa mali

16May 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bilionea amkana mwanawe kisa mali

MFANYABIASHARA mkubwa nchini na mmoja wa wanahisa wa kundi la Kampuni za Motisun, Ramanlal Motibhal Patel, amemkana mtoto wake wa pekee, Veer Ramanial Patel, kwa kile alichodai ni kumdhalilisha kwa kuuaminisha umma kuwa ana ugonjwa wa akili.

Ramanlal Motibhal Patel

Katika tangazo lilitolewa na Patel jana kwenye gazeti moja la kila siku, alisema hamtambui mtoto wake wala hahusiki na kitu chochote, hivyo hatawajibika wala kuhusika na wakopeshaji binafsi, benki, wauzaji na wasambazaji wote wanaofanya biashara ya Motisun Group.

 

"Napenda kuuarifu umma kuwa kuanzia sasa Veer Ramanlal Patel, si mtoto wangu tena wala msimamizi au mdhamini wangu na hausiki na hatahusika na mali zangu zote na masiha yangu nikiwa hai, nitakapokuwa nimekufa, yeye pamoja na mke wake kwa kuwa mimi si baba yake tena," alisema Patel.

 

Akizelezea chanzo cha kumkana kijana wake huyo, Patel, alisema Januari 30, mwaka huu saa 10:30 jioni alipokea notisi za mikutano 35 ya kampuni za Motisun Group ambao ungefanyika Februari Mosi, mwaka huu.

Alisema mkutano huo, ulikuwa na ajenda kuu ya kila notisi ya kumtoa kwenye ukurugenzi wa kampuni zote 35.

Alisema sambamba na hilo, Januari 31, mwaka huu, mtoto wake wa kiume, Veer, kwa nia ovu, alimwomba kupata uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Ilala wa kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Kitengo cha Afya ya Akili ili afanyiwe uchunguzi kwa nia ya kuchukua nafasi yake ya ukurugenzi wa kampuni hizo.

Kwa mujibu wa Patel, lengo la kijana wake huyo ni kutaka kumiliki kampuni hizo kwa kigezo kuwa baba yake ana matatizo ya akili, hivyo hawezi kufanya tena biashara.

"Baada ya uchunguzi wa kina wa madaktari bingwa wa Muhimbili ilibainika kwamba nina akili timamu na sina tatizo la afya ya akili. Wakati nikiwa hospitali kwa siku 17 nilitolewa kwenye nafasi yangu ya ukurugenzi wa kampuni zote na nafasi yangu kuchukuliwa na Veer ili kukamilisha dhamira yao ovu," alisema.

Alisema kutokana na mambo yote aliyofanyiwa, amelazimika kumkana mtoto wake huyo na kwamba hatahusika na kitu chake chochote akiwa hai au endapo atafariki dunia.

Taarifa iliyotolewa jana na mmoja wa watu wa familia hiyo, ilikiri kuwa Ramanlal Patel alikuwa akiugua macho kwa muda mrefu na kumsababisha kutoingia ofisini na kutosimamia miradi, hali inayosababisha kazi zote wafanye viongozi wengine.

Kampuni hiyo na bodi iliamua kufanya vikao na kutokana na hali yake hiyo,  Mzee Ramanlal apumzike kwenye nafasi ya ukurugenzi na abaki na nafasi ya mmiliki wa hisa ili mtoto Veer achukue nafasi ili kampuni iendelee.

Inadaiwa kuwa baada ya taarifa hizo kuvuja, mmoja wa wapambe wake aliungana na wanasheria hao kumshawishi Patel kukataa ombi hilo.

Habari Kubwa