Bilioni 114 kutumika kuleta neema ya maji Dar, Pwani

02Jul 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Bilioni 114 kutumika kuleta neema ya maji Dar, Pwani

MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) imesaini mikataba sita na Benki ya Dunia pamoja na wakandarasi mbalimbali yenye thamani ya Shilingi Bilioni 114 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji kwa jiji la Dar es salaam na Pwani.

Waziri wa Maji Prof Makame Mbarawa akiwasili ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA akiongozana na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja.

Katika halfa hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam katika ofisi za DAWASA, imehudhuliwa na kushuhudiwa na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwa mgeni rasmi, Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jafo, Naibu Waziri wa maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri Mifugo, Abdallah Ulega, Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange, Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia, Wakuu wa Wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani pamoja na viongozi mbalimbali.

Akizungumza katika halfa hiyo, Waziri Mbarawa amesema katika miradi hiyo, DAWASA inatumia fedha zake za ndani Shilingi Bilioni 40 kati ya Bilioni 114 kutekeleza miradi mitano kati ya sita ambapo mmoja kati ya miradi hiyo umesainiwa na Benki ya Dunia.

Amesema mradi wa kwanza kati ya sita ni wa usambazaji wa maji kuanzia kwenye matenki ya chuo kikuu mpaka Bagamoyo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo nafuu ambao utekelezaji wake ni wa miezi 18 mpaka kukamilika." Mradi wa Ujenzi wa bomba la usambazaji wa maji wa 2B na 2F awamu ya pili unatekelezwa na mkandarasi Chengdu Industrial Installation Corporation kutoka China ikishirikiana na Hainan International Ltd (Tanzania)..Kazi ya usambazaji maji itaanzia kwenye matanki ya Chuo Kikuu mpaka Bagamoyo,” Amesema Mbarawa

Amesema kuwa mradi huo wa Chuo Kikuu hadi Bagamoyo unalenga kuhudumia wakazi zaidi 750,000 kulingana na usanifu ambapo wateja wapya zaidi 64,000 wa majumbani wataunganishwa na kuondoa tatizo la maji katika maeneo ya Changanyikeni, Bunju, Wazo, Ocean by Zone, Salasala, Bagamoyo zone na Vikawe zone katika wilaya ya Bagamoyo, Ubungo na Kinondoni.

Amesema kuwa mradi wa pili ni wa kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza ambapo kazi ya ulazaji bomba la km.1.9 imekamilika na kipande kilichobaki cha km. 5.6 DAWASA itanunua bomba kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.

Profesa Mbarawa amesema kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo kutawezesha kubadilisha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam pamoja na Pwani na pia kwa hatua hiyo ya DAWASA kutumia fedha zake za ndani kutekeleza miradi mikubwa mni jambo la kupongezwa kwani ni jambo alilokuwa akitamani kuliona likifanyika ndani ya mamlaka hiyo.

Profesa Mbarwa ametaja mradi wa tatu kuwa ni wa uchimbaji wa visima 20 katika eneo la Kimbiji na Mpera ambavyo vitazalisha maji lita milioni 260 kwa siku ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu ambapo mkakati wa mamlaka umejikita katika kukamilisha visima vya Kimbiji kabla ya kwenda Mpera.

Kwa upande wa Waziri wa TAMISEMI, Suleiman Jaffo, ameipongeza DAWASA kwa kazi nzuri inayofanya katika utekelezaji wa miradi ya maji mbalimbali Dar es Salaam na Pwani.

 “Ukifanya ulinganishi DAWASA inaongoza katika taasisi zote nchini, leo hii tunasaini mikataba ya 114.5 Bilioni za mradi huo, kati ya hizo bil.40 ni mapato ya ndani ya DAWASA sisi tunajua hayo ni mapato ni sawasawa na bajeti ya wizara moja,” amesema Jaffo.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wakandarasi na wahandisi ambao ni wababaishaji kwa sasa hawana nafasi ndani ya wizara yake ambapo hivi karibuni anatarajia kutoa majina yao hadharani.

Amesema kuwa pia orodha ya wahandisi wote wa maji ambao katika maeneo yao wamefanya ubabaishaji mkubwa na hawatakuwa na nafasi tena.

Habari Kubwa