Bilioni 170 kujenga vituo vinne vya Umahiri

24Jul 2021
Augusta Njoji
Dar es Salaam
Nipashe
Bilioni 170 kujenga vituo vinne vya Umahiri

Serikali inatarajia kutumia zaidi ya Sh. bilioni 170 kujenga vituo vinne vya umahiri katika mikoa minne nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Omary Kipanga wakati alipotembelea Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh.bilioni 37 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umahiri wa sekta ya ngozi katika kampasi hiyo.

"Tunataka ifikapo mwaka 2024 tuwe tumekamilisha ujenzi wa Kituo cha umahiri katika masuala ya ngozi, ili sasa tuweze kuzalisha vijana ambao wakimaliza mafunzo yao waweze kuajiriwa au kujiajiri," amesisitiza Kipanga.

 Kipanga ametaja vituo vingine vya umahiri vitakavyojengwa kuwa ni Kituo cha umahiri wa sekta ya anga ambacho kitajengwa katika Chuo cha Usafirishaji (NIT) Jijini Dar es Salaam, kituo cha umahiri wa TEHAMA kitakachojengwa  DIT kampasi ya Dar es Salaam na kituo cha umahiri wa nishati jadidifu kitakachojengwa DIT kampasi ya Arusha.

"Kimsingi Serikali imeamua kwa dhati kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi na umahiri ambao utaleta tija kwenye Tanzania ya viwanda hivyo inakwenda kujenga vituo vinne vya umahiri hadi kufikia mwaka 2024," amesema Naibu Waziri Kipanga.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa DIT, Prof. Praxedius Ndomba amesema kampasi ya Mwanza inajihusisha na mafunzo, utafiti na uzalishaji wa bidhaa za ngozi ikiwemo viatu, mikanda, mabegi na mipira ya kuchezea.

Habari Kubwa