Binti aliyesumbuliwa na uvimbe mguuni, afanyiwa upasuaji, apewa msaada

22May 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Binti aliyesumbuliwa na uvimbe mguuni, afanyiwa upasuaji, apewa msaada

Gazeti la Nipashe pamoja na mitandao yake ya kijamii iliandika habari inayomuhusu Aristidia Bosco (17), mkazi wa Kijiji cha Kamachumu, Kata ya Ibuga,Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera aliyekuwa akisumbuliwa na uvimbe mkubwa katika goti la mguu wa kulia hatimaye afanyiwa upasuaji wa kukatwa mguu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya The Desk and Chair Foundatio, Sibtain Meghjee akimkabidhi vifaa hivyo.

Upasuaji huo umefanyika Mei 20 mwaka huu na kurudisha matumaini mapya kwa mtoto huyo huku Taasisi ya Desk and Chair Foundation ikiendelea kutoa msaada wa matibabu na vifaa wezeshi vya kumsaidia kutembea baada ya mguu kukatwa.

Akizungumza wakati akitoa msaada wa magongo ya kutembelea,baiskeli ya miguu minne pamoja na tende, Mkurugenzi wa Taasisi ya The Desk and Chair Foundatio, Sibtain Meghjee, amesema waliguswa na hali ya mtoto huyo hivyo wanasubiri maelezo ya daktari ili waweze kumsaidia zaidi kwa kumpatia mguu wa bandia huku zoezi la kumsaidia likiwa ni endelevu kwao .

Pia amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kumsaidia mtoto huyo ili aweze kupona na kutimiza ndoto zake.

Kwa upande wake mama mzazi wa Aristidia, Agnes Bosco amesema familia inawashukuru Watanzania waliojitokeza kumsaidia mtoto wake hadi kupatiwa matibabu ya mguu kwani uvimbe huo ulimtesa kwa kipindi kirefu . Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mwanza (MPC) Edwin Soko, amesema hali ya mtoto huyo inaendelea vyema huku akiendelea kutoa shukrani kwa waandishi wa habari hasa Nipashe kwa kujitolea kusambaza taarifa ya mtoto huyo tangu mwanzo na kila hatua anayopiga.

"Alikuwa kwenye wakati mgumu asijue kesho yake kwa sasa nuru imeanza kuonekana tunawaomba watanzania waendelee kujitoa kumsaidia hakika tunatoa shukrani kwa mafanikio haya" amesema Soko.

Kwa yeyote atakayeguswa  kumsaidia Aristidia awasiliane na mama mzazi wa mtoto huyu  kwa namba 0765 494 127 

Habari Kubwa