Binti asimulia alivyowekwa kinyumba na dereva bajaji

23Jan 2018
Renatha Msungu
Nipashe
Binti asimulia alivyowekwa kinyumba na dereva bajaji

MSICHANA mwenye umri wa miaka 13 amesimulia alivyoingia katika mtego wa dereva wa bajaji, James James, na hatimaye kubakwa na kufanywa mke. 

Akisimulia mkasa huo, binti huyo alisema awali alikuwa anafanya kazi katika mtaa wa Chang'ombe, lakini aliamua kuondoka baada ya kutolipwa mshahara wake kutokana na mwajiri kudai anakula sana ndicho kitakuwa malipo yake.

Alisema akiwa kituo cha daladala akisubiri gari ili aondoke, alikutana na dereva huyo ambaye alimweleza kuhusu matatizo yake kisha akamwambia kuna mama anahitaji msichana wa kazi maeneo ya Makulu, Manispaa ya Dodoma.

“Tukaondoka hadi Makulu kukutana na huyo mama, lakini yule mama akasema James anipeleke jioni. Tukaondoka  na  James ambaye alinipeleka kwenye chumba chake Makulu na kuniacha. 

“Aliporudi usiku nilimwuliza mbona hatuendi kwa yule mama, James akadai kuwa ameenda kwa huyo mama akakuta amelewa sana, hivyo wameshindwa kuelewana kwa hiyo nilale kwake hadi kesho ndipo twende,” alisema. Hata hivyo, alisema ilipofika usiku James alimwambia kuwa atakuwa mkewe asimwambie mtu na watu wakimwuliza aseme ni kaka yake, ili waendelee kuishi kama mke na mume.

Alifafanua kuwa usiku alimtaka kimapenzi na akakataa lakini James alimbaka. “Asubuhi aliniachia Sh. 3,000 ili ninunue vitu nipike chakula, lakini nilipokwenda gengeni kununua vitu nilimkuta binti kama mimi anauza genge nikaona nimwelezee yaliyonikuta. Wakati tukiendelea kuongea akatokea mama yake ambaye alimsikiliza na wakashauriana na kinamama wengine, walinipeleka kwenye kituo cha msaada wa kisheria,”alisema. Alisema wahusika wa kituo hicho kwa kushirikiana na polisi walifanikiwa kumkamata James na yeye akapelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alithibitisha jana kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa na sasa yuko mahabusu.   

Habari Kubwa