Binti, waganga kienyeji mbaroni mauaji ya mama

11Jan 2022
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Binti, waganga kienyeji mbaroni mauaji ya mama

SIRI nzito kuhusu mpango wa mauaji ya kikatili ya muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC, Patricia Ibreck (66) imefichuka, baada ya polisi kuanika chanzo cha kifo chake ni kuhoji matumizi ya Sh. milioni 60 za kiinua mgongo chake.

Muuguzi huyo raia wa Tanzania mwenye asili ya Kijerumani, anadaiwa kuuawa mwezi Februari, mwaka jana na mwanawe wa kike na kisha kumzika kwa kificho pembeni ya nyumba yake ndogo iliyoko Kijiji cha Uru-Mkuruti, Kata ya Uru Kusini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Simon Maigwa, hadi kufikia jana mchana, watu watatu walikuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na mauaji hayo.

“Kati ya tuliowakamata wakihusishwa na mauaji haya, yumo mtoto wa kike wa marehemu pamoja na waganga wawili wa kienyeji. Kati yao mganga mmoja anatokea Mkoa wa Tanga na mwingine jijini Dar es Salaam.

“Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuwa waganga hao, walikwenda nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kumpatia tiba mama huyo aliyekuwa mgonjwa. Sasa wakati akiendelea kupatiwa matibabu ya asili, mama huyo alishtukia zaidi ya shilingi milioni 60 za kiinua mgongo alizokuwa nazo zilishatumika na haoni matumaini ya kupona.”

Aidha, Kamanda Maigwa alisema, baada ya mama kuhoji matumizi ya fedha hizo, mwanawe wa kike na waganga hao walikuwa wakimtaka Patricia aende akatoe pesa nyingine na kuzuka purukushani iliyosababisha watuhumiwa hao kuamua kutekeleza mauaji yake.

“Walipomaliza kutekeleza mauaji hayo, waliuchukua mwili wake na kuuhifadhi katika moja ya chumba nyumbani kwa marehemu, wakisubiri giza liingie ili wakachimbe kaburi na kuuzika mwili huo,” alisema.

NDUGU WAHOFU

Kamanda Maigwa, alisema baada ya watuhumiwa kutekeleza dhamira ovu, baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki, walianza kupata shaka ya mwenendo wa mtoto wa kike wa marehemu (hakumtaja jina), kuuza rasilimali, huku mama yake akiwa hajulikani alipo.

Katika taarifa yake, Kamanda alisema binti huyo alianza kuuza mali za mama yake na alipokuwa akiulizwa, alikuwa akijibu anauza ili atume fedha nchini India, ambako mama yake alikuwa akipatiwa matibabu.

Maigwa alifafanua: “Desemba 20, mwaka jana, majirani zake walikuja Polisi kutoa taarifa za shaka kwamba huenda Patricia aliuawa miezi 10 iliyopita. Tulianza uchunguzi ikiwamo kukusanya vielelezo na tulifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa hao ambao walienda kuonyesha walipouficha mwili wa marehemu.

“Ilipofika Januari 9, mwaka huu, tulifanikiwa kuufukua mwili huo na ndani ya kaburi hilo kulikuwa na panga lenye nywele. Baada ya kujiridhisha kwamba ni mwili wa binadamu ulizikwa bila kufuata taratibu, tulichukua mabaki ya mwili huo na kwenda kuyahifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufani ya KCMC, kusubiri uchunguzi wa kina wa kitabibu,” alisema.

Kamanda Maigwa, alisema baada ya uchunguzi wa kina kutoka kwa wataalamu, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalowakabili la mauaji ya kukusudia.

Jana, Nipashe ilifika nyumbani kwa marehemu Patricia na kuwakuta baadhi ya majirani akiwamo Richard Estomii, ambaye alisema enzi za uhai wake Patricia alijaliwa kuzaa watoto wawili mapacha, mmoja akiwa nje ya nchi na mwingine anayetuhumiwa kumuua mama yake.
 
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Musa Lyari, alisema licha ya kutafuta ukweli kwa muda mrefu, binti huyo hakuwahi kuwaonyesha ushirikiano wa alipo mama yake, zaidi ya kudanganya yuko nchini India akipatiwa matibabu.

“Nimemuuliza zaidi ya mara tano kila anapouza viwanja, kila mara anasema anafanya hivyo ili aweze kupata fedha za matibabu kwa ajili ya mama yake aliyeko India," alisema Lyari. 

Habari Kubwa