Biteko aanika ukweli jiwe la rubi Dubai

24Apr 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Biteko aanika ukweli jiwe la rubi Dubai

​​​​​​​MAPYA yameibuka kuhusu jiwe la Rubi linalotajwa kutokea nchini Tanzania lenye kilogramu 2.8 linalotarajiwa kupigwa mnada Dubai ikiwamo baadhi ya nyaraka kuwa na mkanganyiko zikionyesha kuwapo na mawe mengi zaidi.

Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko.

Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko, alitoa ufafanuzi huo jana katika semina ya wabunge ya kuwajengea uwezo kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya Madini iliyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Alisema Aprili 13, mwaka huu, walipata  taarifa kuhusu jiwe hilo na walikwenda kuangalia kwenye taarifa zao za usafirishaji wa rubi lakini hawakuona hilo jiwe.

“Tukawatafuta wahusika SJ ya Dubai tukawauliza tunaomba kujua hili jiwe kawauzia nani kutoka Tanzania kwa sababu linaonekana limetoka Tanzania limekwenda Dubai, mara ya kwanza kwepa zikawa nyingi kama kawaida tukawaambia sasa kama serikali tunataka kutoa taarifa ndiyo wakatoa taarifa juu ya hili jiwe .

“Wakatuambia kwamba hili jiwe halikutoka Tanzania bali limetoka Marekani. Marekani nani kaliuza, wakatuambia muuzaji anaitwa fulani sitaki kumtaja kwa sababu bado tupo kwenye vikao tunaendelea.

“Tukatuma maofisa wetu wa ubalozi wakaenda SJ wakafanya vikao, kikao cha kwanza kikaja na mapendekezo, ni kweli hilo jiwe limetoka Marekani. Lakini limetoka Tanzania, yule Mmarekani kalitoa Tanzania,” alisema.

Alisema wakahitaji nyaraka kutoka kwa huyo Mmarekani kwa kuwa ili kusafirisha madini lazima uwe na cheti halisia na kibali cha kusafirisha kutoka kwenye nchi nyingine.

“Kule wakatuletea certificate ya GIA ya Marekani lakini tukakuta hiyo ‘certificate’ yenyewe ina matatizo, jiwe limetangazwa lina kilo 2.8 lakini certificate waliyotuletea ina kilo 3.4 tukawaambia mbona hii ‘certificate’ ni ya Marekani tuleteeni inayotoka Tanzania.

“Wakasema sisi bwana hiyo ya Tanzania hatuna jana tukakubaliana kufanya kikao Ijumaa Marekani, watu wa SJ Dubai ,ubalozi wetu, sisi pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilipofika mchana wakatuomba tuwape muda wakusanye taarifa zaidi,”alisema na kubainisha kwamba wamewaambia si jiwe hilo wana mawe 12 yametoka Tanzania.

“Tukawaambia basi haina shida  mliyapata lini? wakasema hayo mawe waliyapata miaka 11 iliyopita. Sasa leo asubuhi kwa sababu tumewaambia tunataka kufanya press wametuletea ‘bureau of sell’ badala ya mawe 12 kama walivyosema yapo mawe 25 yenye uzito tofauti tofauti,”alisema.

Biteko alisema kunahitajika utulivu kama taifa kwa kuwa haijulikani dhamira yao ni nini ya kutumia jina la Tanzania kwenye biashara ambayo serikali haifahamu.

“Uungwana ilikuwa hivi sisi kama nchi ambao tume export hata kabla hujasema unataka kufanya mnada na ukakubali limetoka Tanzania basi walau tu uwe unawasiliana na yule ambaye ndio mmiliki origin ambako jiwe linapotokea.”

“Duniani hapa Wabunge madini yana miiko yake yale yanayoingia kwenye masoko ya kimataifa ni yale tu yaliyokidhi vigezo, kigezo cha kwanza ni lazima yatoke kwenye nchi ambayo haina mapigano ya aina yeyote,”alisema.

Alisema kigezo cha pili madini hayo yachimbwe bila kuvunja haki za binadamu na yaaminike.

“Ukisema jiwe hilo limetoka Tanzania kwanza ni nchi ambayo haina mapigano hilo linakuwa salama kwenye masuala ya kimataifa. Kwa hiyo hatujajua dhamira yao ni nini ndio maana tunatamani utulivu uendelee kuwepo achilia mbali kusema Waziri afanye hiki au hiki ni muhimu watanzania wawe na uchungu na mali yao,”alisema.

“Gem Society duniani wale wanaoshughulika na madini yote ya gemology wametoa tangazo kwa kutoa tahadhari kwa wanunuzi kuwa makini na hilo jiwe. Hilo jiwe ni rubi yenye ‘zero site’ wanasema limetoka Winza, jiolojia  haikubali kwa kuwa rubi ya Winza haina ‘zero site’, yenye ‘zero site’ iko Mundalala.

Na pale Mundalala kuna mawe ya aina hiyo mengi mchimbaji mmoja tu anaitwa Sendeu wa Mundalala anayo yale mawe tumeyafunga kwenye kontena na kuyafunga ni tani 8.4. Leo unakuja kuzungumza kilo 2.8 kwa bei ile ni jambo ambalo bado lipo subject to discussion,” alisema.

Aliwaomba Wabunge na Watanzania kuwa watulivu taarifa itakapokamilika watatoa maelezo yenye pande zote mbili.

“Tutatoa nyaraka tutatoa vithibitisho kwa sasa kusema jiwe la nani sijui la nani nadhani ni muhimu taarifa mwishoni itaonyesha ni la nani na mambo gani yapo nyuma yake ili Tanzania tubaki kuwa salama. Nitakuwa Waziri wa ajabu sana kama nitakwenda kulichukua option ambayo baadhi wameitoa kwamba watu wamesema nyie mkubali tutumie jina lenu tutawapa Dola milioni 20.

“Mnatupa Dola milioni 20 kwa kipi tunataka tujue hili jiwe limetoka wapi hiki ni kitu cha msingi halafu mambo mengine yatakuja,” alisisitiza.

Habari Kubwa