Bodaboda kulipwa kiinua mgongo

22Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bodaboda kulipwa kiinua mgongo

MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kesho inatarajia kuzindua fao la huduma za malipo ya kiinua mgongo na pensheni katika sekta isiyo rasmi, wakiwemo waendesha bodaboda.

WAENDESHA BODABODA

Akizungumza katika mktano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Sheria wa SSRA, Oronius Njore alisema mamlaka hiyo imeamua kuwakumbuka wananchi wasio katika sekta rasmi.

Njore alisema sekta hiyo isiyo rasmi, pamoja na waendesha boda boda, inajumuisha pia madereva wa daladala, bajaji na mama ntilie.

Uzinduzi rasmi huo wa fao la huduma za malipo ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi utafanyika jijini Mbeya, Njore alisema.
Njore alisema mwaka 2015 mamlaka ilifanya utafiti katika sekta ya usafirishaji mjini kwa lengo la kubaini ni mfumo gani wa hifadhi ya jamii utawafaa wadau wa sekta hiyo.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha asilimia 83 ya wanaoendesha vyombo vya usafiri mijini wako tayari kuchangia huduma ya mfuko wa hifadhi ya jamii,” alisema Njore.

Matokeo ya utafiti huu, alisema Njore ndiyo yaliyofanya baadhi ya mifuko iwe imekwisha andaa mafao maalum yanayowalenga waendesha bodaboda, bajaji, daladala pamoja na mama lishe.

Alisema wachangia ji hao watapata fursa ya kuweka kiasi kidogo kidogo kwa kila siku kulingana na kipato chao, ili kupata huduma mbalimbali za hifadhi ya jamii kama vile akiba ya uzeeni, matibabu na mikopo.

“Awali jamii ilijenga dhana ya kwamba hifadhi ya jamii ni Huduma maalumu kwa wafanyakazi wa sekta iliyo rasmi pekee, na hasa wenye mikataba ya ajira na hivyo kupelekea wajasiliamali kuona kwamba huduma hiyo si kwa ajili yao," alisema Njore.

"(Lakini) SSRA kwa kuliona hilo, tumeamua kuja na hili kwa waendesha bodaboda ambao wanafikia asilimia 83."

Habari Kubwa