Bodi ya Maji mtegoni ukusanyaji mapato

10Jan 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Bodi ya Maji mtegoni ukusanyaji mapato

WAZIRI wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, ametoa agizo kwa bodi mpya ya maji ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga (SHUWASA), kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato yasiyopungua Shilingi Milioni 700 kila mwezi, na endapo wakishindwa kufanya hivyo ataivunja bodi hiyo.

Waziri wa maji Prof Makame Mbarawa akizungumza kwenye uzinduzi wa bodi mpya ya maji kutoka mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Shinyanga (SHUWASA)

Mbarawa amesema hayo jana Shinyanga mjini alipokuwa akivunja bodi ya zamani ya maji ya mamlaka hiyo iliyomaliza muda wake, pamoja na kuzindua bodi mpya, kuwa hataki ukusanyaji wa mapato legevu hali ambayo inakwamisha ukosefu wa fedha wa kupanua mtandao wa maji na kufikia wakazi wote wa Shinyanga.

Amesema kipimo cha kwanza kwa bodi hiyo mpya ya maji ambayo inaongozwa na mwenyekiti wake Mwamvua Jilumbi, ni kuhakikisha ukusanyi wa mapato unaongezeka si chini ya Shilingi Milioni 700 kila mwezi, fedha ambazo zitasaidia mamlaka hiyo kujiendesha vizuri na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga (Shuwasa) Flaviana Kifizi akizungumza kwenye uzinduzi wa bodi mpya ya maji ya mamlaka hiyo.

“Kazi ya kwanza ambayo natoa kwa bodi hii mpya ya maji (SHUWASA) ni kwamba nataka mkusanye mapato yasiyopungua Shilingi milioni 700 kila mwezi, mkishindwa kukusanya sitakuwa na msalia mtume kuvunja bodi hii”

“Pesa mtakayokusanya muitumie kuilipa mamlaka ya usambazaji maji kutoka Ziwa Victoria (KASHWASA), ili mpanue mtandao wa maji, siyo kila siku mje kuomba fedha Wizarani, fedha mnayopata ipelekeni kwenye miradi, na mjenge miradi hiyo nyinyi wenyewe kwa kutumia wakandarasi wa ndani”,amesema  Mbarawa.

Baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Shinyanga (Shuwasa) wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa bodi mpya ya maji ya mamlaka hiyo.

Pia Mbarawa ameitahadharisha bodi hiyo kutothubutu kutumia fedha za mapato kujilipa posho na kupeana safari zisizo na tija, na kubainisha SHUWASA siyo mahala pa kula fedha, bali ni kwa ajili ya kusaidia wananchi wapate maji safi na ya kutosha.

Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo mpya ya maji Mwamvua Jilumbi, amemtoa wasiwasi Waziri huyo kuwa watahakikisha wanatekeleza maagizo yake ya ukusanyaji wa fedha hizo, huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wateja wa Mamlaka hiyo ya maji, kulipa Ankra zao kwa wakati na kutolimbikiza madeni.

Waziri wa maji Prof Makame Mbarawa akiwa Shinyanga mjini kuvunja bodi ya maji iliyomaliza muda wake na kuzindua mpya kutoka mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Shinyanga, Shuwasa , wa kwanza mkono wa kushoto Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini Stephen Masele, akifuatiwa na mkurugenzi wa Shuwasa Flaviana Kifizi, na mkono wa kulia ni katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Flaviana Kifizi, amesema hivi sasa mamlaka hiyo imeongezewa maeneo mengine matatu ya kutoa huduma ambayo awali yalikuwa yanahudumiwa na RUWASA, ambayo ni Tinde, Didia na Iselamagazi.

Amesema mamlaka hiyo maji (SHUWASA) hukusanya mapato ya wastani wa Shilingi 497,891,531 kwa mwezi, ambapo kiasi hicho cha fedha asilimia tano tu, hutumika katika kuongeza mtandao katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya maji safi na salama, ikiwamo Kata ya Mwawaza.

Waziri wa maji Prof Makame Mbarawa akipiga picha ya pamoja na viongozi mkoani Shinyanga pamoja na bodi mpya ya maji ya mamlaka ya maji Shuwasa.

Habari Kubwa