Bodi ya mikopo yakusanya bil. 94/- kwa nusu mwaka

16Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bodi ya mikopo yakusanya bil. 94/- kwa nusu mwaka

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imekusanya Sh. bilioni 94.01 kutoka kwa wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kati ya Julai na Desemba, mwaka jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul Razaq Badru (katikati), akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kuhusu hali ya ukusanyaji wa fedha za mikopo kutoka kwa wadaiwa kwa kipindi cha miezi sita. Kulia ni Mkurugenzi wa Mikakati na Ubunifu wa Benki ya CRDB, Goodluck Nkini, Mwakilishi wa Mfumo wa Malipo ya Kidijitali, Basil Baligumya (wa pili kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo wa Bodi, Ignatus Oscar. PICHA: GETRUDE MPEZYA

Kiwango hicho kimeelezwa kuwa kimevuka lengo la makusanyo katika kipindi hicho. Bodi hiyo ndani ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19, ilipanga kukusanya Sh. bilioni 71.4.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam kuwa makusanyo hayo yametoka kwa wanufaika 198,659 ambao wamejiajiri au kuajiriwa katika sekta binafsi na umma.

Badru alikuwa akieleza hali ya ukusanyaji wa mikopo katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha wa 2018/2019 unaomalizika baadaye mwezi Juni mwaka huu.
 
“Katika kipindi hicho cha Julai – Desemba, pia tumefanikiwa kuwabaini zaidi ya wanufaika wapya 12,600 ambao walikuwa hawajaanza kurejesha mikopo yao na sasa wameanza, hivyo kufanya wateja wanaorejesha mikopo kufikia 198,656 hivi sasa,” alisema Badru wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za HESLB.

Makusanyo haya ya Sh. bilioni 94.01, alisema ni sawa na ongezeko la asilimia 8.7 ikilinganishwa na Sh. bilioni 85.88 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, yaani Julai hadi Desemba, 2017,” aliongeza.
 
“Malengo yetu kwa mwaka mzima ni kukusanya Sh. bilioni 150, hivyo kwa kukusanya kiasi hicho katika nusu ya kwanza, tunaona tunakwenda vizuri na tutavuka hata lengo letu. Tunawashukuru wateja wetu wanaorejesha na waajiri wanaotuunga mkono kwa kufuata masharti ya sheria,” alisema Badru.
 
Kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha HESLB, waajiri wanapaswa kukata asilimia 15 ya mshahara ghafi wa mnufaika na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB ndani ya siku 14 baada ya tarehe ya mwisho wa mwezi wa makato.
 
Katika hatua nyingine, HESLB pia ilitangaza rasmi kujiunga na Mfumo wa Serikali wa Ukusanyaji Mapato yaani (GePG) na kusisitiza kuwa kuanzia sasa, malipo yote kwenda HESLB yatapokelewa kwa mfumo huo unaofuatwa na taasisi mbalimbali za serikali.
 
“Mwajiri au mnufaika anachotakiwa kufanya ni kunakiri ‘Namba ya Kumbukumbu iliyoko kwenye ankara ya mkopo wake na kufanya malipo kwa njia ya benki au simu,” alisema Badru na kufafanua kuwa namba hizo na maelezo ya kina yamo kwenye tovuti ya bodi (www.heslb.go.tz).

Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango ambao ndio wasimamizi wa GePG, Basil Baligumya, alisema katika mkutano huo kuwa uamuzi wa serikali kukusanya malipo yake kupitia GePG unalenga kumpa mlipaji urahisi wa kulipa, kuongeza mapato na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Nao wawakilishi wa benki za CRDB, NMB na TPB ambao walihudhuria mkutano huo, waliipongeza serikali kwa kuanzisha mfumo wa GePG na HESLB kwa kujiunga kwa wakati na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuwawezesha wateja wa HESLB kulipa kwa urahisi.