Bomoabomoa machinga yachukua sura mpya

20Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bomoabomoa machinga yachukua sura mpya

BOMOABOMOA ya vibanda vya wafanyabiashara wadogo, maarufu machinga, imeendelea kwenye maeneo yaliyokatazwa mkoani Dar es Salaam licha ya uongozi wa mkoa huo kuongeza siku 12 kwa kundi hilo kuyapisha maeneo hayo.

Mwonekano wa barabara ya Nyerere katikati ya Jiji la Mwanza, iliyokuwa imefurika machinga na kusababisha watu pamoja na magari kushindwa kupita, ikiwa wazi kwa sasa, baada ya serikali kuwahamishia kwenye maeneo rasmi. PICHA: VITUS AUDAX

Juzi, Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, alitangaza kuongeza siku 12 kwa wafanyabiashara hao kuondoka kwenye maeneo yasiyo rasmi na kuutumia vizuri muda huo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza muda utakapoisha.

Hata hivyo, Nipashe ilishuhudia jana kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo vibanda vya machinga vikionekana kubomolewa.

Maeneo kulikoshuhudiwa ubomoaji ni pamoja na Tabata, Segerea, Mwenge, Mlimani City, Tegeta, Makumbusho, Temeke, Mbagala, Posta, Gongolamboto, Buguruni na Vingunguti.

Upangaji wa machinga ni moja ya mipango na mikakati ya Makalla aliyoanza kuitekeleza Agosti mwaka huu.

Alisema amedhamiria kuufanya mkoa huo kuwa safi na kurejea katika hadhi yake ya kibiashara.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri, aliiambia Nipashe kuwa wameweka mikakati ili kuhakikisha maeneo yote yaliyosafishwa yanabaki safi na kutoruhusu mtu yeyote kurudi.

Alisema mikakati yao inajumuisha kuweka utaratibu wa kupitisha doria mara kwa mara ili maeneo hayo yawe wazi.

Alibainisha kuwa baadhi ya maeneo watu wanaonekana kuondoa vibanda lakini wanaendelea na biashara kwa kuweka mwavuli, jambo ambalo alisisitiza kwamba haliruhusiwi.

Alisema machinga wote wanatakiwa kwenda maeneo waliyopangiwa na yeyote atakayekaidi, atakamatwa na kufikishwa Mahakama ya Jiji na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Watu watii sheria bila shuruti, muda ulioongezwa na mkuu wa mkoa wautumie vizuri, waondoke katika maeneo yaliyokatazwa ili kuepuka usumbufu na kufanikisha jitihada za serikali katika kulifanya jiji kuwa safi.

"Pia niwapongeze wale ambao wameshaondoka na kuondoa vibanda vyao kwa hiari," Shauri alisifu.

Aliongeza kuwa wameshaongea na kampuni mbalimbali zinazofanya usafi katika mkoa huo na kuingia makubaliano ya kusafisha maeneo yote ambayo tayari wafanyabiashara wameshaondoka na kule ambapo wanaendelea kuhama ili kuhakikisha suala hilo linafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Alibainisha kwamba mpaka jana, kulikuwa na wafanyabiashara watano waliokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kukaidi agizo lililotolewa kwa kurudi na kuendelea na biashara katika maeneo ambayo tayari yalishasafishwa na kuwekewa mabango ya katazo la kufanya biashara.

Habari Kubwa