Bosi Jamii Forums aachiwa akidai uhuru wa habari

20Dec 2016
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Bosi Jamii Forums aachiwa akidai uhuru wa habari

HATIMAYE Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo (40), ameachiwa na vyombo vya dola, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumpatia dhamana jana huku akiwatoa hofu watumiaji wa mtandao huo kuwa hakuna taarifa zitakazodukuliwa kwa kuwa upo salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kukamatwa kwake ni ishara mbaya kwa waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Melo aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa mahakamani hapo na Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. milioni moja kila mmoja.

Alisema anashukuru jamii ya mitandao na vyombo vya habari kutokana na kuibua mijadala iliyoishinikiza Serikali imuachie kwa dhamana.

Alisema kitendo cha kufikishwa mahakamani kilisababishwa na msimamo wake wa kulinda siri za watumiaji wa mtandao huo wa Jamii Forums ambao Polisi walitaka kuudukua.

“Muelewe kufikishwa kwangu mahakamani ni mfano tu, kwani mshishangae mkaona wengine wanafikishwa, lakini hatupaswi kuhofia wala kuogopa, kikubwa ni kulinda siri za watumiaji wa mitandao,” alisema.

Alisema waandishi wa habari wanapaswa kupigania uhuru wa kujieleza ambao upo hatarini kuangamizwa kutokana na sheria mpya ya mitandao kuwa kandamizi.

“Kutiwa kwangu nguvuni ni kama shambulio kwa uhuru wa vyombo vya habari, na ndiyo mara ya kwanza mtu kuwekwa ndani kwa kulinda uhuru wa kuongea. Hii ishara mbaya kwa waandishi wa habari,” alisema.

Hata hivyo, aliwahakikishia watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums kuwa upo salama na hakuna taarifa zozote zilizochukuliwa wala zitakazochukuliwa na mtu yeyote.

“Simaanishi kwamba tunaipinga Serikali, isipokuwa tunapinga sheria dhalimu ya ukandamizaji ambayo tukiendelea kuiachia, itatuangamiza wote kama ilivyoanza na mimi,” alisema.

ILIVYOKUWA MAHAKAMANI

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwambapa jana, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Salum Mohammed, alieleza shauri hilo la Melo namba 457 la mwaka 2016 kuwa limetajwa kwa ajili ya kukamilishwa kwa masharti ya dhamana.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwambapa alisema mshtakiwa huyo anapaswa kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. milioni tano kila mmoja.

Melo alitimiza masharti hayo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Melo anatetewa na Wakili Jebra Kambole na Jeremiha Ntobesya.

Wakili Mohammed alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kuzuia taarifa za upelelezi.

Inadaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Aprili mosi na Desemba 13, mwaka huu kinyume cha kifungu 22(2) cha Sheria ya Mitandao, Namba 14 ya mwaka 2015.

Ilielezwa mahakamani hapo kwamba kosa hilo alilitenda maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media, inayoendesha mtandao wa Jamii Forums.

Ilidaiwa kuwa, Melo, huku akijua kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa makosa ya chapisho za taarifa za mtandao wa elektroniki kupitia tovuti yake, alishindwa kulipa ushirikiano na alizuia upelelezi wa tovuti hiyo.

Hata hivyo, baada ya kusomewa shitaka hilo, Melo alilikana.

Mbali ya kesi hiyo, Melo pia anakabiliwa na kesi ya kuzuia upelelezi kwa Jeshi la Polisi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas Simba.

Inadaiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Aprili mosi na Desemba 13, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa, huku akijua Jeshi la Polisi linaendesha uchunguzi wa makosa ya chapisho ya taarifa za mtandao wa elektroniki kupitia tovuti yake, alishindwa kutoa ushirikiano na alizuia upelelezi wa tovuti hiyo.

Melo alikana kosa hilo na kupewa masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. milioni 10 kwa kila mmoja, ambayo aliyatimiza.

Pia katika kesi nyingine namba 458 ya mwaka 2016, Melo anakabiliwa na makosa mawili likiwamo la kuendesha mtandao usiosajiliwa nchini mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa.

Inadaiwa kosa la kumiliki mtandao ambao haujasajiliwa nchini, alilitenda Desemba 9 na 13, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni Kinondoni jijini.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba, akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd, aliusajili mtandao huo chini ya kifungu 212 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 uliopewa cheti namba 66333 na anaendesha tovuti ya Jamii Forums.com bila kusajiliwa nchini kwa mujibu wa sheria za mtandao (Tanzanian Country Code Top Level Domain -ccTLD) na masuala ya Posta.

Aidha, kwa kosa la kuzuia upelelezi kwa Jeshi la Polisi, inadaiwa Melo alilitenda Januari 26 na 13, mwaka huu, ambapo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co Ltd, unaoendesha mtandao wa Jamii Forums, akijua kwamba Jeshi la Polisi lipo katika uchunguzi wa makosa ya kimtandao zilizochapishwa kwenye tovuti yake, kinyume cha sheria, alishindwa kutoa ushirikiano na kuzizuia taarifa za mtandao huo.

Melo alikana kuhusika na kosa hilo na kuachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. milioni moja kila mmoja.

Melo alikamatwa na Jeshi la Polisi Desemba 13, na kufikishwa mahakamani Desemba 16, mwaka huu na mwishoni mwa wiki alipelekwa mahabusu kwenye gereza la Keko jijini baada kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Habari Kubwa