Bosi mpya Tamwa atoa neno kwa JPM

18Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bosi mpya Tamwa atoa neno kwa JPM

MKURUGENZI mpya wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben, amemwomba Rais John Magufuli, kutenga bajeti ya kimkakati kukabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia unaozidi kushamiri nchini.

Kaimu Mwenyekiti wa Tamwa, Judica Losai (kushoto), akimkabidhi katiba Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Tamwa, Rose Ruben, Januari 11 mwaka huu. PICHA; MAKTABA

Katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Reuben ambaye Januari 19, mwaka huu, alikabidhiwa mikoba ya Edda Sanga (amemaliza muda wake wa miaka mitatu) kukiongoza chama hicho, alisema kuna haja serikali kutenga fungu maalum kukabiliana na changamoto hiyo.

Aliipongeza serikali kwa kuanzisha dawati la jinsia ndani ya Jeshi la Polisi kukabiliana na ukatili wa kijinsia, lakini akasisitiza kuwa bila kuliwezesha, itakuwa ngumu kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na mwandishi wa habari huyo mzoefu:

SWALI: Ukipata nafasi ya kuzungumza na Rais Magufuli kwa dakika mbili, utamwambia jambo gani la msingi?
REUBEN: Nikipata nafasi ya kuzungumza na Rais Magufuli, kwanza nitamshukuru kwa sababu vituo vya polisi vimekuwa na madawati ya jinsia.

Lakini pia nitamwomba kuwa, haya madawati yaimarishwe ili yaweze kufanya kazi yake vizuri ikiwa ni pamoja na kutengewa bajeti inayoweza kuwasaidia kufanya kazi zao vizuri.

Kazi ya dawati la jinsia si nyepesi maana pengine wanakuja watu wamepigwa, wameumia, watu waliolala njaa na kadhalika. Haya madawati yana changamoto nyingi.

Kwa hiyo, ningemwomba Rais katika haya madawati ayaongezee nguvu, yawe na bajeti ya kimkakati ili tuweze kupunguza matatizo ya ukatili wa kijinsia.

Lakini pia ningemkumbusha Mheshimiwa Rais kuwa huu ukatili wa kijinsia unapoongezeka, inakuwa shida kutekeleza sera yake ya 'Hapa Kazi Tu'. Hapa kazi tu inafanywa na mtu ambaye kwa namna yoyote ile haki yake imelindwa, ikiwa ni pamoja na kutengwa na ukatili wa kijinsia.

SWALI: Tamwa umeikuta inakabiliwa na changamoto ipi kubwa na unaitatuaje?

REUBEN: Tamwa kama shirika ambalo linategemea ufadhili, ni moja ya mashirika ambayo yanakabiliwa na changamoto kufanya kazi yake.
Ukiangalia masuala ya ukatili wa jinsia, masuala ya ukeketaji, mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ni vitu ambavyo bado wimbi lake ni kubwa nchini.

Kwa hiyo, Tamwa ingetamani kuwa na jamii ambayo inaangalia na kuthamini haki za binadamu. Kulingana na ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo, Tamwa bado ina changamoto kubwa.

Kwa hiyo, naweza kusema kuwa nimeikuta Tamwa ikiwa na changamoto kubwa ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia maeneo mengi mpaka kufika kule vijijini, bado wimbi ni kubwa.

Unaposikia idadi ya watoto kupotea imeongezeka, basi jua ya kwamba kuna ukatili wa kijinsia mahali fulani, unaposikia kuna wahamiaji haramu wamekamatwa mahali ama watu fulani wamepigwa, basi jua kuna ukatili mahali fulani.

Lakini changamoto nyingine ni katika suala la fedha. Tamwa haina chanzo cha pesa zaidi ya kutegemea kutoka kwa wafadhili, na wafadhili wengi fedha zao wanazielekeza katika malengo yao wanayoyatamani.

Kwa hiyo, ni changamoto nyingine kubwa lakini bado katika kile kidogo tutakachokipata, tutaendelea kukitumia. Tamwa tutaendelea kuhamasisha wafadhili wa ndani na nje ya nchi watambue kuwa nao ni sehemu ya jamii yetu, watuunge mkono kwa kutufadhili ili tuendelee kufanya kazi ya kupiga vita ukatili wa kijinsia.

SWALI: Umekiri ukatili wa kijinsia bado ni changamoto kubwa nchini, Tamwa ya Rose ina mkakati upi kukabiliana nao?

REUBEN: Kwanza nitaiendeleza tulipofikia kwa sababu kuondoka kwa Edda Sanga hakumaanishi kwamba tutaishia alipokuwa amefikia, hapana, nitaiendeleza vizuri na kwa makini sana ili kupate mafanikio makubwa zaidi.

Tunapaswa kushawishi kupata fedha kutoka kwa wafadhili wetu pamoja na jamii kwa ujumla kwa kutumia vyombo vya habari ambavyo vingine ni rafiki na vingine si rafiki katika kuufikia umma kupiga vita ukatili wa kijinsia.

Tunapoona kuwa ukatili wa kijinsia unaongezeka, vifo vinaongezeka, ni wananchi wale. Kwa hiyo, nguvu kazi inaondoka, idadi ya watu waliouana kwa sababu ya wivu wa mapenzi ama kwa kupigwa kwa sababu hakupika, watoto waliobakwa, hiyo ni nguvu kazi ya taifa ambalo mwisho wa siku tunahitaji kuwa na Watanzania ambao watatufikisha katika kuwa na Tanzania ya viwanda.

Tanzania ya viwanda haiwezi kupatikana kwa watu ambao wamebakwa, watu ambao wamepigwa na kuumizwa, inahitaji jamii ya watu wazuri ambao watafanya kazi vizuri.

Nitakachokifanya mimi ni kuendeleza kile kilichopo. Kuendeleza haya mapambano ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa sauti kubwa zaidi, tutatumia vyombo vya habari zaidi, tutatumia kalamu zetu zaidi kuielimisha jamii na kuipasha habari kuhusiana na masuala ya kijinsia. Kwa waandishi wa habari, zile habari zinazoandikwa na kuishia katikati, sasa ziendelezwe.

Habari nyingi za ukatili wa kijinsia zinaandikwa halafu zinaishia katikati, zinaishia katikati eti ooh wameamua kwenda kukubaliana nyumbani ama ati wamesameheana, wamesameheana lakini ule ukatili uliofanyika bado ni kitendo cha kupigiwa kelele na umma.

SWALI: Kwa miaka takribani 30 tangu Tamwa ianzishwe, unafikiri lengo la kuwa na waandishi wengi wanawake kwenye vyombo vya habari nchini limefanikiwa?

REUBEN: Kuwa na waandishi wa habari wengi katika vyombo vya habari kama ilivyo lengo la Tamwa, naweza kusema kuwa limefanikiwa, lakini pia halijafanikiwa na pengine halijafanikiwa kwa sababu kazi ya uandishi wa habari ni utashi, kazi inayotakiwa uwe na bidii.

Tamwa inaendelea kuwatia shime waandishi wote kufanya kazi kwa bidii katika vyombo vyao vya habari na kuendelea kuwatia shime wanawake kushika ngazi za juu zaidi na pia wamiliki wa vyombo vya habari tunaendelea kuwahimiza waangalie waandishi wa habari wapewe kazi kulingana na uwezo wao.

Kwa mfano, wale waandishi ambao ni wanachama wetu, huwa wanahamasishwa kufanya kazi kwa bidii na tunao waandishi wanawake walio katika nafasi za juu na wanafanya vizuri.

Kwa hiyo, licha ya kwamba hatujafikia lengo, lakini ni kitu ambacho tunaendelea nacho katika kuwatia hamasa waandishi wa habari wanawake.

SWALI: Maeneo ya vijijini kuna waathirika wengi wa ukatili wa kijinsia. Tamwa ya Rose ina mkakati gani kuwasaidia wanawake wa vijijini kukabiliana na changamoto hii?

REUBEN: Ni kweli maeneo ya vijijini yana waathirika wengi wa ukatili wa kijinsia na Tamwa ilianzisha mabaraza saba nchini, na tumezifufua kamati za kupinga ukatili na unyanyasaji wa jinsia, maarufu GBV Committee katika wilaya saba Tanzania Bara ambazo ni Kisarawe, Mvomero, Ruangwa, Lindi, Newala, Kitunda na Makumbusho na tatu zingine ziko visiwani Zanzibar.

Kamati hizi zinafanya kazi kubwa ya kuibua madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika maeneo yao.

Lakini pia mkakati wetu ni kuendeleza yale mabaraza kuendelea kushirikiana na serikali za vitongoji, tunatamani kungekuwa na mabaraza kila wilaya au kata ili kuhamasisha, kufunza na kuwaelimisha watu kuwa ukatili wa kijinsia si kitu cha mtu mmoja, bali cha Watanzania wote.

Mkakati wetu ni kuangalia namna gani tunaweza kusogea mbele, haya saba yasiishie pale yalipoishia, tuongeze mengine kulingana na namna tunavyoweza k upata fedha.