Bosi mpya WFP awasilisha hati kwa serikali

22Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bosi mpya WFP awasilisha hati kwa serikali

MWAKILISHI mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson, amewasilisha hati za utambulisho kwa serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, zilizopokelewa na waziri wa wizara hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba Kabudi akiongea na Mkurugenzi Mkazi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)
Sarah Gordon-Gibson leo jijini Dar es Salaam.

“Nina furaha kubwa kurudi Tanzania na kuona kwamba nchi imepiga hatua kubwa katika viashiria muhimu vya maendeleo ya watu na ya kiuchumi,” alisema Gordon-Gibson na kuongeza:

“Tunaendelea kudhamiria kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto zake za kitaifa hususan kuhusu mazingira, tabia ya nchi, skimu za kinga ya jamii, uzalishaji katika kilimo na mifumo ya chakula, mlo kamili na lishe bora, na pia usawa na uwezeshaji wanawake.”

Taarifa iliyotolewa na WFP kwa vyombo vya habari jana, ilisema Gordon-Gibson, ambaye ni mwanasheria kwa taaluma, amefanya kazi na WFP kwa zaidi ya miaka 20. Katika miaka miwili iliyopita, alifanya kazi kama Mwakilishi wa WFP nchini Jordan, ambayo ni miongoni mwa operesheni kubwa za shirika hilo duniani.

Pia, alitumikia kama Mwakilishi wa nchi Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Lao kwa miaka mitatu. Kazi yake ya miaka ya hivi karibuni zaidi ilikuwa ni Naibu Mwakilishi wa nchi za Tanzania, Myanmar na Niger.

Katika kuisaidia Tanzania kufikia nchi yenye uchumi wa kati, WFP inajishughulisha katika maeneo ya lishe, mtandao wa usalama wa kijamii, ugavi wa chakula na kuwasaidia wakulima wadogo. Pia, inawasaidia wakulima hao kupanda ngazi kutoka kufanya kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara na kupata masoko ya uhakika kwa lengo la kuzifanya jamii za wakulima kuwa na usalama wa chakula zaidi, kujitegemea na kuhimili majanga.

Shirika hilo pia linatoa msaada wa chakula kwa wakimbizi na inatafuta njia za kiubunifu za kuleta maendeleo endelevu.

Taarifa hiyo ilisema, WFP pia inafanya kazi za kilojistiki kwa ajili ya nchi zisizopakana na bahari zilizo jirani na Tanzania na ina mchango muhimu katika ukanda wa Afrika Mashariki katika kuwezesha usafirishaji wa chakula ili kuokoa uhai wa watu walio katika migogoro.

“Inashirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania ili kuimarisha nafasi ya nchi kama lango kuu la bahari na mtoaji mkubwa wa chakula katika ukanda huu,” ilisema taarifa hiyo.

Gordon-Gibson alisema WFP ina thamini ushirika wake na Serikali ya Tanzania: “Sehemu muhimu ya ahadi yetu ni kuisaidia serikali kukabiliana na mahitaji ya wale walio na shida zaidi na wasio na usalama wa chakula nchini Tanzania kwa kuleta pamoja utaalamu, uwezo na rasilimali zetu na kushirikiana zaidi kuliko hapo kabla ili kumaliza njaa na utapiamlo hadi ifikapo mwaka 2030.”

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya 2020.

“Ndiyo shirika kubwa zaidi la kibinadamu, tunaokoa maisha katika dharura na tunatoa msaada wa chakula kujenga amani, utulivu na ustawi kwa watu walioathirika na mizozo, maafa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.”

Habari Kubwa