Bosi Tanapa aibiwa Millioni 9 Simiyu

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Simiyu
Nipashe
Bosi Tanapa aibiwa Millioni 9 Simiyu

Mkuu wa Kikosi kazi cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Ziwa ambaye pia ni Mhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanapa, Richard Shilunga inadaiwa kuwa ameibiwa Shilingi Milioni 9.4 akiwa katika nyumba za kulala wageni Bariadi mkoani Simiyu.

kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Deusdedit Nsimek, picha Happy Mollel

Ilidaiwa kuwa Shilunga aliwasilia kwenye nyumba moja inayofahamika kwa jina la Sumaye 'Lodge' iliyopo katikati ya mji wa Bariadi, Janauri 13, 2019 majira ya saa 10 jioni akitokea Tarangire Mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa moja ya chanzo cha taarifa hiyo, kilieleza kwamba Shilunga alifika katika nyumba hiyo, akiwa na begi dogo ambalo linadaiwa kuwa na kiasi hicho cha fedha ambazo bado haijafahamika kama zilikuwa za matumizi ya kitu gani.

Aidha, Shilunga baada ya kuwasili alipewa chumba herufi T, ambacho gharama yake ni Shilingi 20,000, na kuhifadhi begi lake kisha akatoka na kwenda kutazama mchezo wa mpira wa mguu wa ligi Kuu ya Uingereza kati Manchester United na Tottenham.

Baada mchezo huo kuisha, majira ya 2:45 usiku Shilunga alirejea katika nyumba hiyo na kuingia kwenye chumba chake,na baadaye kabla ya kulala aligundua kupotea kwa kiasi hicho cha fedha na kutoa taarifa katika kituo cha Polisi Bariadi.

Hata hivyo haikujulikana fedha hizo kama zilikuwa mali ya serikali au zake binafsi, huku ikidaiwa kuwa hakuweza kutoa taarifa kwa wahudumu wa nyumba hiyo kama ana kiasi hicho cha fedha.

Polisi wadhibitisha na kuingia mashaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo ambao walifika katika kituo kikuu cha polisi, baada ya kupata taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Deustedith Nsimeki alikiri kuwepo kwa tukio hilo, na uchunguzi unaendelea.

Kamanda Nsimeki amesema mpaka sasa wanawashikilia watu ambao ni wahudumu wa nyumba hiyo, ambao hata hivyo hakutaka kuwataja majina yao kwa sababubu za kiupelelezi.

“Tukio kweli yupo mtu anaedai kupotelewa na fedha hizo mtumishi wa Tanapa kituo cha Tarangire mkoani Manyara. Bado tunaendelea na uchunguzi ili kubaini kama fedha zilizoibiwa ni mali ya Serikali, Kama tutabaini ni kweli mali ya serikali watamfungulia mashitaka kwa mwendesha mashitaka wa serikali kwa sababu ya uzembe, kuna taratibu za kubeba pesa kiasi kikubwa ziwe za Serikali au mtu binafsi,”alisema Nsimeki.

Amesema kuwa bado wana mashaka juu ya kuibiwa kwa pesa hizo kama ni kweli au hapana, kutokana na taarifa za awali zikieleza kuwa mlalamikaji kutotoa taarifa za mdomo au maandishi kwa wahudumu kama ana kiasi hicho cha pesa.

Amesema kuwa taarifa za awali zinaeleza kuwa Shilunga alikuja na pesa hizo kwa ajili kuwalipa baadhi ya watu walioko kwenye kikosi kazi maalumu kanda ya ziwa.

“Kwa kawaida pesa za serikali huziendi hivyo wala huwezi kubeba kama kwa njia hiyo kuna mifumo yake hata kama ni ulipaji bado kuna mifumo yake, hata fedha binafsi kuna taratibu, lakini huyu hakuna sehemu ambayo ametoa taarifa kama ana kiasi hicho cha fedha,” Nsimeki.

Aidha Kamanda Nsimeki amesema kuwa mbali na kuwashikilia wafanyakazi hao kwa ajili ya uchunguzi, bado kuna wasiwasi kama kweli ameibiwa fedha hizo kutokana na taarifa za awali.

Aliongeza kuwa watafanya uchunguzi wa kina kufahamu ukweli wa jambo hilo kama kweli mlalamikaji aliibiwa, lakini kujua kama za serikali au hapana, lengo lake lilikiwa nini? Lakini pia kujua kwa nini anatemebea na kiasi kikubwa cha pesa.

Aliwataka wananchi au watumishi wa serikali wenye tabia za kubeba kiasi kikubwa cha fedha, kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za ubebaji wa fedha za kiwango hicho ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea hasa kuibiwa au kuvamiwa.

Habari Kubwa