BoT: Huduma za kibenki kutofungwa uchaguzi mkuu

16Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
BoT: Huduma za kibenki kutofungwa uchaguzi mkuu

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema huduma za kifedha zitaendelea kutolewa kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, jijini Dar es Salaam, huduma  za kibenki zinazotolewa na benki na taasisi za fedha nchini kutolewa kama kawaida.

“Benki Kuu inawataka wananchi kupuuza taarifa potofu zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba kuna maelekezo ya kusitisha huduma hizo muhimu katika kipindi cha uchaguzi,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilisema kama msimamizi wa benki na taasisi za fedha, haijatoa maelekezo yoyote ya kusitisha huduma za kibenki kwa wateja wa taasisi hizo.

“Wananchi wataendelea kupata huduma zote za kibenki kama kawaida wakati wote kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi,” ilisisitiza taarifa hiyo huku ikitoa onyo kwa wapotoshaji.

Habari Kubwa