BOT kuwekeza sehemu salama

23Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe
BOT kuwekeza sehemu salama

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema itaendelea kuwekeza katika Taasisi salama na kwenye Amana zilizo salama ili kulinda thamani na usalama wa akiba ili kuwezesha Serikali kulipia mahitaji mbalimbali ikiwemo deni la Taifa

Fidelis Mkatte

Akizungumza katika semina ya waandishi wa habari za Uchumi, Biashara na Fedha katika tawi la Benki Kuu ya Tanzania BoT Mtwara, Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, Fidelis Mkatte amesema fedha za Taifa ni lazima kuwekezwa kwenye Amana ambazo ni salama kwa kuwa haiwezekani kuwekeza sehemu ambazo hazitoi faida. "Kuna miongozo ya uwekezaji wa fedha, ni lazima uwekeze kwenye vitu ambavyo ni salama kwa kuwa ni fedha ya nchi, huwezi kuwekeza sehemu ambayo haitotoa faida hivyo tunawekeza sehemu salama na tunawekeza dhamana ya Serikali za nchi nyingine kama vile Marekani, Uingereza na Australia kupitia makundi mbalimbali ya fedha ikiwemo dola." Amesema Mkatte. Aidha, Mkatte amesema, Benki kuu ndio yenye dhamana ya kutunza hazina ya Fedha za kigeni za nchi kwa niaba ya Serikali kwa kuziwekeza kwenye mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha kwa faida. "Benki Kuu ina sera za kutoa miongozo ya fedha za kigeni pamoja na uwekezaji wa fedha za kigeni kwa kuzingatia usalama na hutumia hazina hiyo ya fedha ya kigeni kufanya malipo ya nje ya nchi kutokana na majukumu mbalimbali yanayofanywa na Serikali mfano malipo ya ndege." Amesema Mkatte.

Habari Kubwa