BoT yapiga marufuku kodi, ada VICOBA

24Feb 2021
Salome Kitomari
Mtwara
Nipashe
BoT yapiga marufuku kodi, ada VICOBA

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema hakuna tozo au ada yoyote inayotakiwa kutozwa na mamlaka yoyote ya serikali kwenye usajili wa vikundi vidogo vya fedha hususan VICOBA.

Aidha, vikundi ambavyo vimetozwa fedha au vitatozwa fedha za usajili na halmashauri au manispaa yoyote vinatakiwa kutoa taarifa BoT ili hatua zichukuliwe.

Pia vikundi vimetakiwa kutokuwa chini ya mdhamini au Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS), bali vitatakiwa kusajiliwa moja kwa moja na halmashauri au manispaa pekee na kupewa cheti cha usajili ambacho kinatolewa bure.

Ufafanuzi huo ulitolewa jana na Meneja wa Huduma Ndogo za Fedha na Maduka ya Kubadilisha Fedha, Victor Tarimu, wakati akiwasilisha mada ya usimamizi wa watoaji huduma ndogo za fedha mjini Mtwara kwa waandishi wa habari wanaohudhuria mafunzo ya kuandika habari za uchumi, biashara na fedha.

Alitoa ufafanuzi kutokana na maswali ya waandishi wa habari juu ya uwezo wa taarifa za kutozwa kodi kwenye fedha za wanachama kila mwezi na mwisho wa mwaka.

“Hakuna fedha yoyote itayotozwa kodi kwenye mtaji ya wakopaji wala faida waliyoyapata wanakikundi mwisho wa mwaka,” alifafanua.

Alisema usajili wa VICOBA bado haujaanza kwa kuwa walisubiri mwongozo wa mfumo wa kujaza taarifa za kikundi na kwamba vimekamilika ikiwamo kutoa elimu kwa maofisa maendeleo ya jamii ambao wanawajibu wa kutangaza katika maeneo yao usajili unaanza lini.

“Kumekuwa na maneno mengi ila taarifa rasmi ya BoT ni kuwa hakuna kikundi kinalazimika kuwa chini ya SACCOS au mdhamini. Kinachotakiwa wasajiliwe na wafuate matakwa ya kisheria,” alisema Tarimu.

“Halmashauri au Manispaa hairuhusiwi kutoza fedha yoyote kwa kikundi. Kuna taarifa tulipata kuwa kuna vikundi vilitozwa Sh. 30,000 ya usajili. Ikitokea wakituandikia tutafuatilia na fedha zao zitarudi. Usajili hadi kupata cheti ni bure na hairuhusiwi kutoza fedha yoyote.

“Bila mifumo ingekuwa shida maana maofisa maendeleo ya jamii hawakuwa na elimu, wakitoka kwenye mafunzo ndani ya mwezi mmoja hadi miwili wanatakiwa wawe wamesajili vikundi. Kinachotakiwa kwa vikundi ni idadi ya wanachama, viongozi, katiba na muhtasari wa wanachama kuanzisha kikundi,” alisema na kuongeza:

“Usajili unachukua saa mbili na baada ya hapo ndani ya siku 14 kikundi kinatakiwa kiwe kimepata cheti cha usajii kilichosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri husika.”

MADARAJA NA WALIOSAJILIWA

Kwa mujibu wa meneja huyo, kuna madaraja manne yaliyotambuliwa kisheria na kila moja lina kanuni zake na mamlaka iliyokasimiwa kusimamia.

Alisema daraja la kwanza ni benki zinazotoa huduma ndogo za fedha ambazo zinasimamiwa na BoT.

Daraja la pili ni taasisi zinazotoa mikopo bila kupokea amana za umma ikijumuisha kampuni za kukopesha, watoa huduma ndogo kwa njia za kudijitali na watu binafsi wanaokopesha.

Aidha, alisema hadi sasa wamepokea maombi 663, leseni 293 zimeshatolewa na mengine yamekataliwa na baadhi yako katika hatua za usajili hadi Februari 2, mwaka huu.

Alibainisha kuwa zaidi ya waombaji wa kampuni binafsi za ukopeshaji baada ya kupewa masharti hawakurudi na wengi hawakuwa wamesajiliwa Brela na BoT kupata leseni ya kazi husika.

Alisema daraja la tatu ni la vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) ambavyo usimamizi wake umekasimiwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), na hadi sasa kuna maombi 241 kati ya 1,000 zilizopo.

Meneja huyo alisema kuwa daraja la nne ni la vikundi vya huduma ndogo za fedha vya kijamii (VICOBA, VSLAs), ambayo usimamizi wake umekasimiwa kwa mamlaka za serikali za mitaa.

Alisema utaratibu huu unakwenda kukabiliana na wagopaji sugu kwa kuwa taarifa za watu zitakuwapo kwenye mfumo ambao benki, taasisi za fedha, saccos na vikundi vitaona.

“Mfumo huo utaonyesha mwenendo wa mkopaji, kama amekopa sehemu A na anavyorejesha, lakini itaonyesha hata ankara mbalimbali anazolipa au halipi kama za maji, umeme, ni mfumo mzuri utasaidia sana kuepukana na mikopo chechefu,” alisema.

ADA KWA WATU BINAFSI/KAMPUNI

Kwa mujibu wa kanuni ya sheria ya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2017, watoa huduma ndogo za fedha wasiopokea amana ikiwamo kampuni za mikopo, watu binafsi wanaokopesha na wakopeshaji kwa njia ya kidijitali watatakiwa kulipa Sh. 500,000 kwa kampuni na Sh. 300,000 kwa watu binafsi.

Habari Kubwa