BoT yapiga marufuku uuzaji noti chakavu

25Feb 2021
Salome Kitomari
Mtwara
Nipashe
BoT yapiga marufuku uuzaji noti chakavu

BENKI Kuu (BoT) imepiga marufuku biashara ya kuuza fedha chakavu, ikizitaka benki na taasisi za fedha kutoa fedha safi na kurudisha kwao zilizo chafu ili ziondoke kwenye mzunguko.

Meneja wa benki hiyo anayeshughulikia noti na sarafu, Ilulu Ilulu, alitoa agizo hilo jana wakati wa semina kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara inayoendelea mjini Mtwara.

Alisema katika maeneo ya masoko na minada kumekuwa na watu ambao wananunua fedha chakavu kwa bei pungufu na kwenda kubadilisha BoT kwa bei kamilifu kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, fedha inabadilishwa kwa fedha kamili.

"Hairuhusiwi kuuza fedha chafu, tunataka wananchi kutoa taarifa, fedha inabadilishwa kwa fedha. Tuna sera ya kuhakikisha tunatoa noti na sarafu chafu kwenye mzunguko na kuhakikisha safi zinapatikana.

"Taasisi za fedha zinajua, zinapaswa kuja BoT kuchukua noti safi na kurudisha chafu ambazo tuna jukumu la kuziharibu kisheria," alifafanua.

Alisema wanachofanya wauzaji, wanazikusanya kwa bei pungufu, akitolea mfano noti ya Sh. 10,000 wanazinunua kwa Sh. 9,000, hivyo wakizifikisha BoT, wanapata faida ya Sh. 1,000 kwa kila noti.

Habari Kubwa