BoT yaridhishwa na mwenendo wa uchumi

15Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
BoT yaridhishwa na mwenendo wa uchumi

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya taifa ya fedha pamoja na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa dunia kwa Julai na Agosti, mwaka huu, kutokana na kuongezeka kwa ukwasi katika tasnia ya benki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na benki hiyo, uwapo wa ukwasi wa kutosha katika kipindi hicho kwenye tasnia ya benki umejidhihirisha katika viwango vya riba katika masoko ya fedha ambavyo vimeendelea kubaki kati ya asilimia tatu hadi tano.

Pia taarifa hiyo ilisema mikopo kwa sekta binafsi ilikuwa kwa asilimia 4.1 kwa mwaka ulioishia Julai, kutoka asilimia 3.6 kwa mwezi uliotangulia.

“Kamati imebaini kuwa ukuaji wa uchumi wa dunia unaendelea kuimarika licha ya  janga la corona, japo kwa kasi ndogo na unatarajiwa kuendelea kuimarika siku za usoni. Mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa robo ya kwanza ya mwaka 2021, ulikuwa wa kuridhisha.

“Uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 4.9, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, uchukuzi, kilimo, uzalishaji viwandani na uchimbaji wa madini. Uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 2.2, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.5 katika robo ya kwanza ya mwaka 2020,” ilisema taarifa hiyo,

Kuhusu mfumuko wa bei, taarifa ilieleza kuwa umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia tatu hadi tano sawa na malengo ya kitaifa na vigezo vya mtangamano wa kikanda huku sekta ya utalii ikiendelea kukabiliwa na vikwazo vinavyotokana na corona wakati mauzo ya dhahabu yakitajwa kuongezeka kufikia dola za Marekani bilioni tatu kwa mwaka ulioishia Julai, 2021.

Akiba ya fedha za kigeni imetajwa kuendelea kubakia katika viwango vya kuridhisha na kufikia dola za Marekani bilioni 5.5 na kwamba kiasi hicho kinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa zaidi ya miezi sita, sawa na lengo la nchi na makubaliano ya jumuiya za kikanda.

“Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi ulikua kwa asilimia 11 kwa mwaka ulioishia Julai 2021, ukiwa ndani ya lengo la ukuaji wa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka 2021/22, mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka, japo kwa kasi ndogo ya asilimia 4.1,” ilibainisha taarifa.

Habari Kubwa