Boti ‘bubu’ zafichuliwa Geita

23Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Geita
Nipashe
Boti ‘bubu’ zafichuliwa Geita

ZAIDI ya boti 250 katika Ziwa Victoria mkoani Geita, zikiwamo za kusafirisha abiria na uvuvi, zinatoa huduma hizo bila kusajiliwa na hivyo kukiuka kanuni, taratibu na sheria zinazosimamia usafiri wa majini nchini.

Akizungumza wakati wa kampeni maalum ya elimu ya kanuni za usalama wa vyombo vya usafirishaji majini katika mialo ya Nkome, Mchangani na Makatani wilayani Geita juzi, Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) mkoani Geita, Rashid Katonga, aliwataka wamiliki wa boti hizo kuzisajili kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, Mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa na zaidi ya boti 1,000 zinazotoa huduma ya usafirishaji katika Ziwa Victoria.

Hata hivyo, alisema boti 750 zikiwamo za uvuvi pamoja na zinazosafirisha abiria na mizigo zimesajiliwa na hivyo kufanya kazi zake kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.

“Kutosajiliwa kwa zaidi ya boti 250 kumeilazimu TASAC kutoa elimu kwa wamiliki wa boti kuhusu umuhimu wa kuthibitishwa kwa ubora wa chombo husika,” alisema.

Ofisa Kitengo cha Uratibu na Uokoaji Ziwa Victoria, Joseph Mkumbo, alisema wastani wa ajali mbili hadi tatu hutokea kwenye Ziwa Victoria kila siku na kugharimu maisha ya watu.

Alisema sababu kuu ni ubovu wa vyombo vya usafiri pamoja na ubebaji wa abiria na mizigo kupita kiasi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Emmanuel Ndomba, alibainisha mpango wa ujenzi wa vituo 10 vya kuratibu shughuli za ufuatiliaji na uokoaji katika Ziwa Victoria.

Habari Kubwa