Brela yaja na nyenzo kulinda kazi za wabunifu, wafanyabiashara

02Jul 2022
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Brela yaja na nyenzo kulinda kazi za wabunifu, wafanyabiashara

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imezindua nyenzo ya tathmini ya miliki bunifu itakayowawezesha wafanyabiashara na wabunifu kulinda kazi zao wanazozitengeneza na kufanya uamuzi sahihi katika matumizi ya haki hizo.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Andrew Mkapa.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Andrew Mkapa, amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya uzinduzi wa nyenzo hiyo iliyohusisha taasisi za serikali na vyama vya wafanyabiashara waliopata fursa ya kufundishwa ili kuifahamu.

Anasema Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Miliki Bunifu (WIPO) ambao wamewasaidia kutengeneza nyenzo hiyo ya kieletroniki ambayo itatumika kwa njia ya mtandao kwa wajasiriamali au wafanyabiashara wanapotaka kupata taarifa fulani zinazohusiana na miliki bunifu.

“Kama mtu atataka kusajili alama yake ya biashara au ubunifu wake ulindwe, nyenzo hii ndiyo atakayotumia ambayo ndani yake ina maswali na inatoa majibu na kutoa ripoti ambayo mjasiaramali au mfanyabiashara atafanya uamuzi sahihi ya kile anachotaka kukifanya,”  anasema.

Mkapa anasema hiyo ndiyo moja ya faida ya nyenzo hiyo kumrahisishia mjasiramali na mbunifu badala ya kutembea taasisi mbalimbali kutafuta taarifa, atazipata mtandaoni.

Awali, akisoma taarifa ya Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa kwa niaba yake, Mkapa anasema katika kusimamia jukumu hilo na kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa mashirika ya kikanda ya kimataifa ya wamiliki bunifu, wanashirikiana nao katika kuendeleza na kusimamia masuala hayo nchini.

Anasema kwa kushirikiana na WIPO, wakala inatekeleza miradi mbalimbali ya wamiliki bunifu na huo ni mmojawapo wa kuratibu nyenzo ya tathmini ya miliki bunifu kwa wafanyabiashara na wabunifu.

“Nyenzo hii ambayo tumeitambulisha kwenu leo ambayo wataalam wa BRELA watawapitisha, imeandaliwa na WIPO kwa minajiri ya kuwawezesha wafanyabiashara na wabunifu kufanya tathmini haki  katika biashara zao na kufanya uamuzi sahihi katika matumizi ya haki hizo,” anasema.

Anafafanua kuwa kwa kutumia nyenzo hiyo itawezesha walengwa kulinda kazi za ubunifu walizotengeneza au kuwa katika nafasi nzuri kisheria wanapoamua kutumia bunifu za watu wengine au kuwapa haki ya matumizi watumiaji wengine ambao ama wanamahusinao ya kibiashara au wanataka kuhamisha haki zao.

Anasema wanatangaza nyenzo hiyo kwa taasisi hizo ambazo zinafanya kazi na wabunifu ambao kimsingi wana bunifu nyingi ila bado hawajazitambua au hawafahamu namna ya kuziendeleza kwa manufaa ya biashara zao.

Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Miliki Bunifu BRELA, Seka Kasera anasema nyenzo hiyo wameipata kwa msaada wa WIPO baada ya Tanzania kupitia kikao cha wakuu wa taasisi wa miliki bunifu duniani kilichofanyika mwaka jana kuona kuna tatizo kwenye wabunifu na wafanyabiashara.

Anaongeza kuwa waliona kuna tatizo kwenye kupata taarifa sahihi za miliki bunifu ambazo zinahusisha bunifu za usajili biashara na huduma, vumbuzi na haki miliki ambapo mtu anapotaka kuzilinda walionekana kuna matatizo.

Anasema wabunifu walikuwa wakienda kutafuta ushauri, wakati mwingine ulikuwa siyo sahihi na hutumia muda mwingi kufanya utafiti na gharama wanapokwenda kwa mawakili na wataalam.

“Kwa kushirikiana na WIPO wametupa nyenzo ambayo ukiingia inakuuliza maswali, unaweza unataka kutengeneza tovuti ya biashara, itakuuliza ni aina gani ya tovuti na aina ya biashara na walengwa ni kina nani, ukimaliza nyenzo itakuwa maelekezo taratibu za kufuata kama ni kuilinda kisheria uende taasisi gani."Hii hata wasanii itawasaidia,”anaeleza.

Anasema nyenzo hiyo itasaidia kupunguza muda, gharama na kupata taarifa sahihi kwa sababu wengi waliokwenda BRELA walikuwa wanakwenda na kitu ambacho hawakukitarajia.

Anasema nyenzo hiyo kwa sasa wameipata kwa lugha ya kiingereza na kwa kwa kushirikiana na WIPO lengo ni kufikia watu wa chini hivyo wameshafanya tafsiri yake.

“Mtu yupo Singida ana mafuta ya alizeti anataka kuwa na alama yake ya biashara ili aingie kwenye soko la kimkoa, kitaifa au kimataifa mjasiriamali huyu atumie nyenzo hii. Kama mnavyojua uchumi wa nchi upo kwa wajasiriamali,  tunawezaje kuwafanya kulifikia soko la kitaifa na kimataifa lazima tuwe na nyenzo hii,” anabainisha.

Anasema wameanza kutoa taarfa hizo kwa baadhi ya taasisi za umma na baadae watazunguka nchi nzima ili wananchi wapate huduma hiyo ambayo inatolewa bure.

Habari Kubwa