Bugando yaweka historia upasuaji nyonga, magoti

10Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bugando yaweka historia upasuaji nyonga, magoti

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dkt Fabian Massaga, amesema Hospitali ya Bugando imeweka historia kwa kuanza kutoa huduma ya upasuaji wa kubadili nyonga na magoti.

madaktari wakifanya upasuaji.

Dkt. Massaga amesema tangu Julai 6,2020 hadi leo Julai 10 hospitali hiyo imefanya upasuaji huo ambao hapo awali ulikuwa ukifanyika katika Taasisi ya Mifupa (MOI) pekee. 

"Julai 6, 2020 tulianza uchunguzi na tulipata wagonjwa wengi zaidi ya 250 na kati ya hao wagonjwa 20 walihitaji upasuaji wa haraka,kambi hii ya nyonga na magoti (Total hip and knee replacement) imefanyika kwa ushirikiano mkubwa sana wa Hospitali ya MOI na Bugando", amesema Dkt Massaga.

Aidha Dkt. Massaga ametoa shukrani kwa Mkurugenzi wa  MOI kwa kutoa madaktari kwenda Bugando kwa ajili ya zoezi hilo.

Kwa upande wa Dkt Billy Haunga, kutoka MOI amesema, watu wengi wanaopata matatizo ya nyonga na magoti ni wazee, watu waliopata mivunjiko ya paja au nyonga, wahanga wa ajali na wagonjwa wa selimundu.

Pia amepongeza uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kuanzisha huduma hiyo ya kubadili nyonga na magoti ambayo itaondoa adha kwa wagonjwa wa Kanda ya Ziwa na mikoa ya jirani kusafiri na kwenda Dar es Salaam au nchi za nje kufuata matibabu.

Naye Dkt Inyasi Lawrence Akaro, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mifupa na Mkuu wa Idara ya Mifupa Bugando ameshukuru uongozi wa Bugando na Taasisi ya Mifupa MOI kwa kufanikisha upasuaji huo wa nyonga na magoti ambao utakuwa endelevu katika hospitali hiyo.

Habari Kubwa