Bulaya  aunga  kina  Mbowe

17Apr 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bulaya  aunga  kina  Mbowe

IDADI ya washtakiwa katika kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeongezeka na kufikia tisa, baada ya upande wa Jamhuri kumuunganisha  Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, na kusomewa mashtaka 12.

Vingozi tisa wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, akiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa kwanza kulia) na Katibu Mkuu Vicent Mashinji (wa tatu kushoto), wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa kesi inayowakabili ya kuhamasisha maandamano. PICHA: HALIMA KAMBI

Mbali na Bulaya, washtakiwa wengine ni Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Musoma Mjini, Esther Matiko,  Katibu Mkuu, Vincent Mashindi, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime, John Heche.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi na Dk. Zainabu Mango uliomba mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Willibard Mashauri, kubadilisha hati ya mashtaka kwa kumuunganisha mshtakiwa mmoja. Hakimu alisema hana pingamizi na ombi la Jamhuri. 

Nchimbi alidai shtaka la kwanza, kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu Bulaya na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu  Bulaya  alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui Kinondoni kwa kushawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Bulaya alikana na Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na uliomba kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali. 

Hata hivyo,  Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alidai washtakiwa karibu wote ni wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na wenzao wawili ni Manaibu Katibu wakuu wa Chadema Zanzibar na Bara.

Alidai shtaka la pili linalowakabili katika hati ya mashtaka linakiuka haki ya msingi ya washtakiwa ya kufanya shughuli za kisiasa za chama chao. Kibatala alidai upande wa mashtaka kwa makusudi kusema kuwa Februari 16,2018 ilikuwa ni siku ya kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni na kwamba ni shughuli halali ya kisiasa, vivyo kuomba kuipeleka kesi hiyo Mahakama Kuu ili iweze kutoa tafsiri iwapo ni halali kwa washtakiwa hao kushtakiwa kijinai.

Kibatala alidai pia katika shtaka la nne hadi la tisa, anaomba mahakama iridhie wapeleke mahakama Kuu suala la kikatiba kwa sababu watu kutoa maoni yao kuhusu mwenendo wa nchi ni haki yao.

Aliongeza katika  mashtaka hayo hakuna mahali ambapo upande wa mashtaka umesema maneno yaliyotamkwa na washtakiwa ni ya uongo ama ni ya kutungwa.

Kibatala aliongeza upande wa mashtaka uwapatie vielelezo hivyo kupitia mawakili wao, ili kuwawezesha washtakiwa kufahamu kwa ufasaha mashtaka yao ili wajue yapi wanayakubali yapi wanayakataa.

Naye Wakili Jeremiah Mtobesya anayewatetea washtakiwa hao, pia alisisitiza ili washtakiwa wapewe fursa ya kusikilizwa kikamilifu, ni lazima waelewe kikamilifu nini hasa amefanya ambacho kinakiuka sheria.

Baada ya hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu,Faraja Nchimbi, alidai kilichowasilishwa na upande wa utetezi kisheria hakina mashiko na kuomba kujibu hoja hizo leo.

Aprili 5, mwaka huu Mbunge wa Tarime Vijijini,  John Heche, aliunganishwa katika kesi hiyo kwa kusomewa mashtaka matatu ikiwamo kufanya mkusanyiko usio halali na kutoa lugha ya chuki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wake.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu  barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa. 

Habari Kubwa