Bunge lakunwa mradi wa umeme

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bunge lakunwa mradi wa umeme

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza serikali kwa kutekeleza mradi wa umeme wa Makambako-Songea (KV 220) ambao umewezesha Mikoa ya Ruvuma na Njombe kupata umeme wa uhakika kutoka Gridi ya Taifa.

Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti Mariamu Ditopile, ilitoa pongezi hizo wilayani Songea mkoani Ruvuma mwishoni mwa wiki, baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo unaohusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo KV 220 kutoka Makambako hadi Songea, ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea na usambazaji umeme katika vijiji 122.

Kabla ya kukagua kituo cha kupoza umeme cha Songea, kamati hiyo ilikagua vituo vya Makambako na Madaba pamoja na njia ya usafirishaji umeme kutoka Makambako hadi Songea, watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme (Tanesco) wakitoa maelezo ya mradi huo kwa wajumbe wa kamati.

Pamoja na pongezi hizo, Ditopile aliagiza wizara na Tanesco kuhakikisha wanapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyopangwa kupelekewa huduma hiyo kupitia mradi huo na kutoruka kijiji chochote ambacho kimepitiwa na mradi.

Kiongozi huyo wa kamati pia aliiagiza wizara na shirika hilo kuhakikisha wanahamasisha wananchi kutumia umeme huo kwa matumizi mbalimbali kwa kuwa mikoa hiyo sasa ina umeme wa kutosha na wa uhakika na serikali inahitaji wateja wengi zaidi ili kuongeza mapato.

Awali, katika kituo kupoza umeme cha Makambako, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kaleman, aliieleza kamati hiyo kuwa mradi huo ulikamilika mwaka 2018 na kazi inayoendelea sasa ni usambazaji wa umeme katika vijiji vya awali 122 na tayari vijiji 105 vimeshaunganishwa nishati hiyo.

Dk. Kalemani aliongeza kuwa mradi huo umetekelezwa na Tanzania kupitia Tanesco kwa kushirikiana na Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida), ukigharimu Sh. bilioni 216 na kwamba wateja wa awali 22,000 watafaidika na mradi huo.

Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga, alisema miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme (kV 220) imejengwa kwa umbali wa Km 250 na nguzo 711 zimesimikwa.

Aliongeza kuwa kufika kwa umeme wa Gridi ya Taifa katika mikoa hiyo, kumefanya wananchi wahamasike kutumia umeme huo, akibainisha kuwa awali matumizi ya umeme kwa Mkoa wa Ruvuma yalikuwa ni takriban MW tisa, lakini sasa yameongezeka na kufikia MW 11.

Habari Kubwa