Bunge lapigwa shule mkataba biashara EU

07Nov 2016
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Bunge lapigwa shule mkataba biashara EU

WABUNGE wamepatiwa semina kuhusu Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya(EPA), huku wasomi na wataalamu wakitahadharisha Tanzania iangalie faida na hasara kabla ya kuingia kwenye mkataba ambao huenda ukaligharimu Taifa.

Katika ratiba ya vikao vya bunge inaonesha Alhamisi Bunge litajadili na kuishauri serikali kuhusu mkataba huo.

Waatalamu hao waliitoa tahadhari hiyo jana kwenye semina hiyo iliyofanyika kwa wabunge wote mjini hapa.

Walisema ni vyema wabunge wakasoma vizuri na kuangalia maudhui ya mkataba huo kama yanakidhi matakwa ya kibiashara na kiuchumi kwa nchi kabla ya kuupitisha.

Akichambua maeneo tata ya mkataba huo kwa wabunge, Profesa Palamagamba Kabudi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema mkataba huo unamapungufu mengi kwa Tanzania kibiashara na kiuchumi hivyo nchi inahitaji muda mwingi wa majadiliano ili kujua faida itakayozipata kwenye mkataba huyo.

“Tunaweza kufanya maamuzi magumu ya kuukataa mkataba huu kama ulivyo kwasasa hauna faida kwetu kwa maslahi kwa Taifa lakini nyie kama wabunge mnayo nafasi ya kuusoma kwa kina na kujadiliana ili kufanya maamuzi sahihi,” alisema Prof. Kabudi.

Mtaalamu huyo alisema EPA ina maslahi makubwa kwa nchi nyingine ambazo tayari zimekwishausaini na kuupitisha katika mabunge yao.

“Asilimia kubwa ya uchumi wa nchi hizo hasa viwanda una mkono wa nchi za Ulaya na ndio maana haikuchukua muda kwa baadhi ya nchi kutia saini kwa kuwa una maslahi kwao.”

Hata hivyo, aliwapitisha katika ibara mbalimbali za mkataba huo ambazo zinaonyesha kuwa ni mbaya na haufai Tanzania.

“Ukiingia kwenye mkataba wa EPA hauruhusiwi kuongeza ushuru na unainyima nchi fursa ya kuendeleza viwanda vyake vidogo,” alisema mtaalamu huyo.

Aidha, Prof. Kabudi alisema EPA inatoa ahadi kuwa endapo Tanzania ikifungua mipaka yake uchumi utakuwa mzuri lakini ahadi hiyo haiwezi kuleta muujiza bali itaathiri biashara Afrika.

“Mkataba una mitego mingi na kasoro nyingi, haufai na si mzuri nchi yetu na sitaweza kuwashawishi usainiwe.”

Mtaalamu mwingine kutoka UDSM, Dk. John Jingu, akichambua athari za EPA kiuchumi, alisema utakuwa chanzo kikubwa cha kuathiri masoko kwa kuwa hata Tanzania ikiingia mkataba, Ulaya si wanunuzi wa bidhaa zetu.

“Tanzania inauza bidhaa zake na kupata mitaji kutoka nchi za Uingereza, India, Kenya, Netherland (Uholanzi), China, Marekani, Afrika Kusini na si nchi za (Umoja wa EU) Ulaya hivyo ni vyema suala hili likaangaliwa na kujadiliwa kwa kina,” alisema Dk. Jingu.

Alisema kama Tanzania itaingia kwenye EPA uwezo wa kupata mitaji utapungua na nchi itapoteza asilimia 10 ya ushuru.

Aidha alisema kuna mbunge mmoja nchini Ujerumani alisema Mkataba wa EPA ni sawa na kuwanyooshea Waafrika bunduki katika vifua vyao na kwamba endapo Tanzania ikiusaini itakuwa imejimaliza yenyewe.

“Nchi za Carribean wameingia tangu mwaka 2009, ripoti inaonesha pamoja na mambo mazuri lakini imepata hasara Euro milioni 353-498,” alisema mtaalamu huyo.

Kwa upande wake, Dk. Ng’waza Kamata kutoka UDSM alisema mkataba huo haufai na hautaisaidia nchi kukua kisasa, kitaifa na kujitegemea ila uamuzi ni uamuzi wa wabunge kuipeleka nchi peponi au jehanamu.

Dk. Kamata aliwataka wabunge kufanya maamuzi kwa manufaa ya nchi na Watanzania kwa ujumla.

Alisema wabunge ndio wenye dhamana ya kuifanya nchi isonge mbele kwa kukuza uchumi wa nchi yake au kuirudisha nchi kule ilipotoka.

Wakichangia katika semina hiyo, wabunge walionekana kuuponda mkataba huo na kudai kuwa ni mbovu huku wakishauri serikali kuweka utaratibu wa kuleta mikataba mibovu ili wabunge waweze kujadili.

Mbunge wa Ilala (CCM), Musa Zungu alisema mikataba ya aina hiyo inaweza kuingiza nchi kwenye masuala ya ushoga huku akisema hauzungumzii maslahi yeyote kwa Tanzania kama masuala ya korosho na chai.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini (chadema), Peter Msigwa alishauri pamoja na kuzifahamu hasara za mkataba huo ni vyema wakapatikana wataalamu wa kueleza kwa kina faida ili nchi ifanye maamuzi sahihi.

Mbunge wa Ubungo (chadema), Saed Kubenea alisema jambo hilo lisiamuliwe kiushabiki na kwamba wataalamu wamesema Tanzania itapoteza kodi lakini kuhusu uwekezaji bado haifahamiki.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe alisema ni haki kwa Tanzania kuukataa mkataba huo na kwamba Kenya wamesaini kwasababu ya maslahi yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Makete(CCM), Profesa Norman Sigala, alisema ni vyema wabunge wakafahamu hakuna mkataba duniani unaoweza kumbeba mdhaifu na ukawa na faida kwake.

Alisema maendeleo ni vita na kama Tanzania haitaki pia serikali iweke mikakati ambayo itaweza kuipaisha nchi kiuchumi na si kupitia EPA.

“Kenya anasaini kwa sababu zake. Huu mkataba hakuna soko huria lisilo na masharti tufanye kitu kuokoa hilo,” alisema Mbunge huyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalum (CCM), Anatropia Theonest alisema inawezekana Tanzania inapata kigugumizi kuusaini kwasababu nyuma ya pazia China imezuia kuingia kwenye mkataba huo.

Naye, Mbunge wa Kigoma Mjini(ACT-wazalendo), Zitto Kabwe, alisema mkataba wa EPA unahitaji mjadala mpana kwa kuwa unaonesha faida ni ndogo na hasara ni kubwa.

Habari Kubwa