Bunge lataka wasimamizi wa uchaguzi kuwajibishwa

03Apr 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Bunge lataka wasimamizi wa uchaguzi kuwajibishwa

BUNGE limeutaka uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwawajibisha wasimamizi wa uchaguzi wanapobainika kufanya uzembe unaosababisha madhara katika uchaguzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa, picha mtandao

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa, alitoa rai hiyo bungeni jijini hapa juzi alipowasilisha taarifa na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema kuna haja tume hiyo kufuatilia mienendo ya wasimamizi wake wa uchaguzi na kuchukua hatua dhidi ya wanaobainikia kufanya uzembe na kutozingatia sheria, kanuni na taratibu.

"Kamati inaendelea kushauri kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ihakikishe inafuatilia wasimamizi wake wa uchaguzi na kuwawajibisha pale wanapofanya uzembe unaosababisha madhara ambayo yangeweza kudhibitiwa mapema na msimamizi aliye makini na anayetambua na kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria," alisema.

Mbunge huyo wa Rufiji (CCM), pia alisema kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa ushauri wake kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa uangalifu mkubwa.

Hata hivyo, akasema kamati inaendelea kuishauri NEC kujitahidi kufanya kazi yake kwa weledi ili kuendelea kuaminika kwa wadau wake wa uchaguzi, na hasa kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Alisema kamati yake pia imeridhishwa na jinsi Hazina ilivyotoa fedha kwa wakati kuiwezesha tume kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura, lakini bado inaendelea kuishauri serikali kuhakikisha inatoa fedha zinazoidhinishwa na Bunge kwa wakati ili kuiwezesha tume hiyo kuratibu masuala mbalimbali ya uchaguzi kwa ufanisi mkubwa.

Nayo Kamati ya Bajeti iliishauri kujengwa kwa ofisi za wabunge majimboni na kuziwekea samani ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi wanapokuwa majimboni.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mashimba Ndaki, alisema kamati yake inaona kuna haja utekelezaji wa suala hilo ufanywe kupitia Mfuko wa Bunge na siyo kukasimiwa kwa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Alisema kamati yake pia inashauri kuwe na bima ya afya kwa wabunge baada ya ukomo wa Bunge kwa kuwa bima walizonazo kwa sasa zitakoma Juni 30, mwaka huu mara tu baada ya Bunge la 11 kuvunjwa.

Alisema wanaona lazima kuwe na utaratibu wa wabunge kuwa na bima katika kipindi cha miezi minne kuanzia Julai hadi Oktoba mwaka huu, wabunge wapya watakapoapishwa.

Habari Kubwa