Bunge latengua kanuni kuruhusu viongozi kuingia ukumbuni

22Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bunge latengua kanuni kuruhusu viongozi kuingia ukumbuni

Bunge la Tanzania leo Alhamisi Aprili 22, 2021 limetengua kanuni ya 160 (1) ya kanuni za kudumu za chombo hicho cha kutunga sheria ili kuruhusu baadhi ya wageni kuingia ukumbini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama, ametoa hoja ya kutengua hoja hiyo kufuatia ujio wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye leo atalihutubia Bunge.

Kabla ya hoja hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai ameeleza kuwa ujio wa rais utakuwa na wageni wengi hivyo baadhi watalazimika kuingia ndani ya ukumbi kutokana na unyeti wa nafasi zao.

Akisoma orodha ya wageni watakaoingia ukumbini Ndugai amesema ni makamu wa Rais, Dk Philip Mpango; Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi; Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais Zanzibar.

Wengine ni jaji mkuu wa Tanzania, jaji mkuu wa Zanzibar, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki na Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Rais Samia inakuwa mara ya kwanza kulihutubia bunge tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dk. John Magufuli aliyefarki mwezi Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa