Burunge: Jumuiya hifadhi inayosimama kwa mtindo wa bajeti mabilioni

07Jul 2020
Salome Kitomari
BABATI
Nipashe
Burunge: Jumuiya hifadhi inayosimama kwa mtindo wa bajeti mabilioni
  • *Iko na vijiji 10, kimoja kina Sh. mil. 500
  • *Vina shule, zahanati, nyumba za walimu...

NI nadra kwa kijiji kuwa na uwezo wa kutimiza huduma za kijamii kwa kutumia mapato yake, huku kikiwa na akiba Sh. milioni 500 benki zinazosubiri kupangiwa matumizi ya maendeleo.

Diwani wa Kata ya Mwada, Gerald Chembe, akionyesha jengo la bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mbungwe, wilayani Babati, mkoani Manyara. PICHA: SALOME KITOMARI

Lakini, unapotembelea vijiji 10 vya Kata za Nkaiti, Mwada na Magara katika Tarafa ya Mbugwe wilayani Babati mkoani Manyara, utayaona makubwa ya huduma za kijamii kama majengo ya shule, nyumba za walimu, zahanati, vituo vya afya na ofisi za vijiji za kisasa, ni vigumu kupata mfano wake katika vijiji vingine.

 

Katika vijiji hivyo, pia kuna ushuhuda wa ujenzi wa majengo ya shule mpya na huduma nyinginezo za kijamii. Siri ya mafanikio hayo ni nini? Fedha zinazotokana na utalii, kwenye Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (Burunge Wildlife Management Area -WMA).

 

Ni kwamba, kila kijiji kinanufaika na mgao wa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kutekeleza maendeleo yao kwa mujibu wa vipaumbele walivyojiwekea.

 

Nipashe ilifanya ziara ya kuchunguza kupata undani wa uhalisia huo kwa uwezeshaji wa Shirika la Internews chini ya Mtandao wa Waandishi wa Habari Duniani (Earth Journalist Network).

 

Sura pana ya manufaa hayo, imebainika kuwezeshwa kujiendeleza kielimu kwa ngazi mbalimbali kwa watoto kutoka familia zisizojiweza kiuchumi. Hapo kuna maana ya ngazi kama vyuo vya ufundi hadi kileleni vyuo vikuu.

 

Kimsingi, kitaifa kuna jumla ya jumuiya 38. Kati yake, 16 ndiyo zimesajiliwa, ambazo mbali na Burunge, nyinginezo ni Iyumbu, Ipole, Ikona, Makao, Enduiment, Wami Mbiki, Ukutu, Tunduru, Mbaragandu, Liwale, Ngarambe Tapika na Idodi Pagawa.

 

Burunge inashika nafasi ya pili kimapato ikikusanya Sh. bilioni 2.3, ikitanguliwa na Serengeti inayokusanya Sh. bilioni 2.7 kwa mwaka.

 

Katibu wa Jumuiya ya Burunge, Benson Maise, anafafanua utaratibu wa mgao wa mapato, kwamba nusu hubaki kwenye jumuiya kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na kinachobaki hupelekwa kwenye vijiji 10 vilivyo katika ubia na hifadhi hiyo.

 

Tafsiri ya mafanikio yaliyoko vijijini, ni kwamba vinamiliki hoteli za kitalii zenye wateja mamia ya wageni hifadhini, ambazo manufaa yake yanaenda moja kwa moja kijijini.

 

Mfano hai wa mafanikio hayo, unaonekana katika Kijiji cha Sangaiwe chenye akiba ya Sh. milioni 500 benki kwa ajili ya matumizi kama vile ujenzi wa shule, zahanati na miradi ya barabara na maji.

 

Katibu huyo anafafanua vigezo vya mgao, inapotokea kijiji kinashindwa kutunza eneo la hifadhi, kinanyimwa fedha hizo hadi kitakaporekebisha kasoro zilizojitokeza.

 

Mafanikio yaliyopo hadi sasa, wakazi wa vijiji vyote 10 hawachangishwi fedha za miradi ya maendeleo kama ilivyowahi kujitokeza huko nyuma katika hatua za kujipanga walipochangisha Sh. 70,000 kwa kila kaya.

 

Maise anasema, kwa sasa akiba ipo na kinachofanyika ni fedha zinatumika kwa mujibu wa bajeti na mipango iliyopitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.

 

DIWANI ANENA

Diwani wa Mwada, Gerald Chembe, ambako ndiyo makao makuu ya WMA, anasema vyombo vya usafiri vilivyopo, pia vinatumika kuwapeleka wanavijiji katika mahitaji kama hospitali, shughuli za kiuchumi na kijamii.

 

Chembe ambaye yumo katika waanzilishi wa WMA hiyo, anasema walianza na wazo la uchumi wa uhifadhi na wakalitekeleza kwa kutoa elimu kwa kushirikiana na Africa Wildlife Foundation, na wakapata mwitikio wa wananchi ambao waliridhia sehemu ya ardhi yao kuingizwa kwenye jumuiya.

 

"Tulianza kama hifadhi ya jamii, nami nilikuwa katibu wa kamati ya usimamizi wa mazingira. Tulipeleka baadhi ya wananchi kusoma, wakati huo tulikuwa tunatembea porini kwa miguu na baiskeli na bado baadhi walikuwa hawaoni umuhimu kwa kuwa waliendelea kukata miti na kulisha mifugo.

 

"Kuna vitu tuliruhusu kama wazee anapotaka miti kwa ajili ya shughuli za kienyeji na hupewa kibali na kusindikizwa na askari, na waliruhusu kunapokuwa na shida ya kuni kwa ajili ya shughuli za jamii, kijiji kinaandika barua anaruhusiwa kuokota kuni kavu," anasimulia.

 

Diwani anakiri manufaa waliyopata, mbali na kuni, wakazi walipata dawa na mahitaji mengineyo katika kata hiyo yenye vijiji vitatu na baada ya kupatikana wawekezaji kwenye WMA, biashara ya utalii ilianza mara moja na mapato yakaanza kuonekana, huku kukiwapo manufaa ya moja kwa moja vijijini.

 

 

"Mgao wa sasa ni zaidi ya Sh. milioni 100 kwa kila kijiji. Tunakaa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) na kuainisha vipaumbele vya kila kijiji na tunakwenda kwenye mkutano wa kijiji kuwaeleza na baada ya kupitishwa, fedha hutolewa kwa usimamizi wa halmashauri," anafafanua.

 

Anaeleza utaratibu uliopo, kila mamlaka iliyoidhinishiwa matumizi, fedha huwekwa kwenye akaunti yake, mathalani akaunti za shule zinazosimamiwa na bodi ya shule kutekeleza mradi, chini ya kamati ya ujenzi.

 

"Kutokana na fedha hizi katika Shule ya Sekondari ya Mbugwe, tumejenga matundu 36 ya vyoo, madarasa, hosteli na miundombinu ya shule. WMA ilitoa Sh. milioni 19 za ukarabati wa madarasa matatu na madawati 100. Kwa ujumla, miradi ya shule hiyo ni zaidi ya Sh. milioni 300. Kwa sasa tunajenga bwalo litakalotumiwa na wanafunzi 1,000," anasema.

 

Chembe anafafanua wamejenga vyoo vya kisasa vinavyokidhi mahitaji ya makundi yote shuleni, wakiwamo watu wenye ulemavu.

 

"WMA imesaidia kusukuma maendeleo kwa haraka zaidi kuliko kata zilizozunguka Halmashauri ya Babati. Nguvu ya halmashauri kugawa fedha kwa kata 25 ni ngumu sana. Ubunifu huu umevifanya vijiji vyetu kufanya maendeleo kwa fedha zao.

 

"Uhifadhi umetuwezesha wananchi kujua kukata miti, kuua mnyama ni vibaya na ndiyo maana wanyama wapo. Ukitembelea kata yangu, tumefanya miradi mikubwa, utadhani fedha zimetoka Serikali Kuu, kumbe ni faida ya uhifadhi,” anasema.

 

Anaendelea kuwa WMA ilikofikia sasa, ni hatua ya kuwekeza kwenye miradi mikubwa, kama ujenzi wa shule, huku ikimiliki magari na trekta, huku halmashauri nayo ikinufaika kwa mgao wa zaidi ya Sh. milioni 200 kwa mwaka.

 

MWENYEKITI KIJIJI

Lawrence Mukebe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwada, anasema fedha walizopata tangu mwaka 2012, zimewazesha kujenga ofisi kubwa ya kijiji, akijigamba ikiwa na ubora wa kipekee katika Halmashauri ya Babati yenye huduma kama ukumbi, stoo, ofisi ya mtendaji wa kijiji, masjala na ofisi za wataalamu.

 

Anataja miradi ya maendeleo na kiasi cha fedha kilichotolewa katika mabano kwa kila mradi ni: Madarasa matatu ya Shule ya Msingi Mbugwe (Sh. milioni 44.3); choo (Sh. milioni 26.7); mfumo wa maji (Sh. milioni 3.5); na ukarabati wa zahanati ya kijiji (Sh. milioni 33).

 

Mingine ni: Kukarabati maabara (Sh. milioni 3.7); choo cha shule ya sekondari (Sh. milioni 18); hosteli (Sh. milioni 16); jengo la utawala (Sh. milioni tisa); umeme kwenye madarasa (Sh. milioni 9.9); na kukamilisha ujenzi wa nyumba mbili za walimu, ambazo wanakijiji walitakiwa kuchangia maji katika ujenzi.

 

Anadokeza mipango inayoendelea mwaka huu ni: Kujenga madarasa mawili; ofisi ya walimu; umeme ofisi ya kijiji; ujenzi wa nyumba ya matabibu wawili na huduma ya umeme.

 

"Serikali ya kijiji tunashiriki kulinda eneo ulilolitoa na kuunda WMA. Tunatunza, tunakamata mifugo na wanatozwa faini kulingana na taratibu tulizojiwekea. Hatufanyi mradi wowote bila kushirikisha wananchi, ni lazima wapitishe kwenye mkutano mkuu wa kijiji," anasema.

 

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbugwe, Justine Ndikile, anaunga mkono kwamba jumuiya imewezesha shule kuwa na miundombinu bora, yakiwamo madarasa ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

 

“Tayari kijiji kimepitisha miradi ya kipaumbele kwa mwaka huu kuwa ni kujenga ghala la mazao na kuingiza umeme kwenye madarasa yote. Walimu wana makazi, zote hizi ni kutokana na nguvu za uhifadhi zinazofanywa na jamii," anasifu.

 

ITAENDELEA KESHO

 

Habari Kubwa